Makala

MWANAMKE MWELEDI: Ushawishi wake haupingiki kamwe

August 17th, 2019 2 min read

Na KEYB

ANAPIGIWA upatu kuwa mmojawapo wa watu wenye akili zenye thamani kubwa humu nchini, sifa ambazo zimetambulika hata kimataifa.

Sifa hizi zimemtambulisha Ory Okolloh katika baadhi ya majukwaa yanayotamaniwa.

Kwa mfano mwaka wa 2011, Bi Okolloh alitambuliwa kama kiongozi chipukizi katika ‘World Economic Forum’.

Aidha mwaka wa 2014 jarida maarufu la ‘Time Magazine’ lilimjumuisha miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa ulimwenguni.

Sio hayo tu kwani mwaka wa 2015 alikuwa mmoja wa Wakenya sita walioshirikishwa kwenye Quartz Africa Innovators, orodha ya wabunifu barani Afrika iliyoandaliwa na jukwaa la kidijitali la habari la Quartz.

Mwaka huo huo kampuni ya Thompson Reuters Founders Share Company inayoongoza kwa taarifa za biashara na wataalamu ilimteua katika bodi ya wakurugenzi.

Lakini hatambuliki tu kwa ukwasi wake kiakili ambao umemfanya kuhudumu katika baadhi ya mashirika makuu kimataifa, Bi Okolloh pia amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya uanaharakati na kutetea haki za kibinadamu.

Yeye ni mwanzilishi mshiriki wa Mzalendo, mtandao unaotumka kuchunguza shughuli za Bunge. Aidha, yeye ni mwanzilishi wa Ushahidi, mtandao unaotumika kurekodi ushahidi wa visa vya ukiukaji haki za kibinadanu kupitia arafa, barua pepe, Twitter na Google Maps.

Kumbuka kwamba teknolojia hii iliyoundwa na kutumika na wavuti huu pia imetumika kukagua uchaguzi mkuu nchini, mwendo wa trafiki na dhuluma za kisiasa katika mataifa mbalimbali.

Ana shahada ya digrii katika masuala ya sayansi ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Pittsburgh, Amerika na shahada ya digrii ya sheria katika chuo kikuu cha Harvard Law School nchini humo humo.

Ni ustadi huu ambao umempa fursa ya kualikwa kama msemaji katika warsha mbalimbali. Bi Okolloh amehutubu katika warsha kama vile TED Talk, World Economic Forum, Clinton Global Initiative na Mobile Web Africa.

Katika warsha hizi, mada za hotuba zake zilihusisha ukusanyaji, usambazaji na udadisi wa habari kupitia umma hasa kwa njia ya mtandao (citizen journalism), teknolojia barani Afrika, na majukumu ya vijana katika harakati za kuunda picha ya Afrika katika siku za usoni.

Yeye pia ni mwanachama wa bodi ya Africa Media Initiative, kamati ya kudadisi huduma zinazotolewa na Benki ya Dunia (World Bank Service Delivery Indicator Committee), Baraza la watu maalumu katika Benki ya Dunia (the World Bank’s Council of Eminent Persons) na mwanachama wa bodi ya ushauri ya Code for All, mwunganisho wa kimataifa wa mashirika yanayoamini kwamba mtandao unafungua njia kwa raia kushiriki katika masuala ya umma.

Pia, amehudumu katika mashirika mbalimbali ya haiba ya juu kama vile Covington and Burling, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (Kenya National Commission on Human Rights) na pia kama mwanachama wa ushirika wa Chayes (Chayes Fellow) katika idara ya madili ya kitaasisi katika Benki ya Dunia (World Bank Department of Institutional Integrity).

Kabla ya kujiunga na kampuni ya Google, ambapo alikuwa msimamizi wa uhusiano wa sera za umma na uhusiano wa serikali wa Afrika, Bi Okolloh tayari alikuwa mwanzilishi mshiriki wa mtandao wa Mzalendo na Ushahidi. Alihudumu kama mkurugenzi mtendaji wa Ushahidi tangu ilipoanzishwa mwaka wa 2010.

Kwa sasa yeye ni mkurugenzi wa uwekezaji katika shirika la Omidyar Network’s Governance na Citizen Engagement Initiative in Africa, wadhifa aliouchukua baada ya kuondoka kutoka kampuni ya Google.