Kimataifa

Mwanamke mwingine ajifungua watoto 6 kwa dakika 9

March 17th, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

Houston, Amerika

MWANAMKE mmoja kutoka Amerika amejifungua watoto sita kwa kwa mpigo kwa kipindi cha dakika tisa pekee.

Bi Thelma Chiaka ambaye ni mkazi wa Houston alijifungua watoto wanne wa kiume na wawili wa kike mnamo Jumapili katika Hospitali ya Wanawake ya Texas.

Wahudumu wa hospitali walisema watoto hao wamewekwa katika kitengo cha kuwatunza watoto wachanga ambako wataendelea kuhudumiwa. Walizaliwa kati ya saa kumi na dakika 50 na saa kumi na dakika 59 alfajiri.

Tukio hilo linajiri siku tano baada ya Bi Evelyn Namukhula kutoka Kaunti ya Kakamega, Kenya kujifungua watoto watano mara moja kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya kaunti hiyo.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 28 alijifungua wavulana wawili na wasichana watatu.

Hata hivyo, watoto hao walihamishwa hadi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret baada ya wawili kati ya kupatwa na matatizo ya kupumua.

Mama Namukhula ni mkazi wa kijiji cha Sikokhe katika eneo bunge la Navakholo. Mumewe ambaye anajulikana kama Herbert Nambwire ni kiziwi na husaka riziki kwa kufanya kazi za vibarua kijijini Sikokhe.

Hata hivyo, Bi Thelma Chiaka amempiku Bi Namukhula kwa idadi ya watoto wanaozaliwa kwa mpigo  mwaka huu.