Habari Mseto

Mwanamke sasa ataka mazishi ya Murunga yasimamishwe akidai ni mkewe

November 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE anayedai kuwa mke wa mbunge wa Matungu Justus Murunga Makokha aliyefariki siku tano zilizopita amewasilisha kesi katika mahakama ya Milimani kusimamisha mazishi.

Bi Agnes Wangui Wambiri anadai kwamba ndoa yake na marehemu ilibarikiwa na watoto wawili.

Anaomba hatima ya watoto aliopata na marehemu iamuliwe sawia na kugawiwa urithi pamoja na watoto wa wake wengine.

Bi Wangui amewashtaki wake wenza Christabel Murunga na Grace Murunga pamoja na wasimamizi wa mochari ya Lee Funeral.

Wangui anaomba mahakama iamuru sampuli za DNA zitwaliwe kutoka kwa mwili wa mwanasiasa huyo kuchunguzwa kubaini kwamba ndiye baba wa watoto hao wawili wenye umri wa miaka saba na mitatu.

Kupitia kwa wakili Danstan Omari, Wangui anayeomba kesi hiyo iratibishwe kuwa ya dharura amefichua walianza uhusiano wa kimapenzi na Murunga alipokuwa msimamizi wa kampuni ya kuuza mashamba ya Embakasi Ranching.

“Tulianza uhusiano wa kimapenzi na hatimaye tukaanza kuishi pamoja katika mtaa wa Utawala Nairobi,” asema Bi Wangui katika ushahidi aliowasilisha katika mahakama ya Milimani.

Alipochaguliwa kuwa Mbunge 2017, kitumbua chao kiliingia mchanga lakini aliwakodishia nyumba na amekuwa akigharamia mahitaji yao.

Anahofia atazuiliwa kushiriki katika mipango na mazishi ya Murunga aliyeaga Novemba 14,2020 baada ya kuugua kwa muda mfupi.