Habari MsetoSiasa

Mwanamke wa kwanza kuongoza wanafunzi UoN, uchaguzi wa utulivu TUM

April 8th, 2019 1 min read

NA STEVE MOKAYA

Juma lililopita lilikuwa na shughuli kabambe, hasa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Hii ni kwa sababu wengi wao walipata fursa ya kuwachagua viongozi wao.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN)walimchagua kiongozi wa kike kwa mara ya kwanza tangu muungano wa wanafunzi kuanzishwa.

Hayo yakitendeka jijini Nairobi, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) nao waliwaacha maafisa wa usalama vinywa wazi kwa utulivu wao.

Bi Ann Mwangi Mvurya, mwanafunzi wa Uanasheria mwenye miaka 24, alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa muungano wa wanafunzi UoN.

Ann Mwangi Mvurya akila kiapo. Picha/ TWITTER @vcuonbi

Ann amenakiliwa katika kumbukumbu kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhfa huo, kwani katika miaka yote ya huko nyuma, kiti hicho kilikuwa kikikaliwa na wanaume.

Na si wanaume hivi hivi tu, bali wale wenye sauti na uwezo hata wa kukabili serikali. Ni wanaume wenye nguvu ya pesa na usemi mkali. Hivyo basi, uchaguzi wa Bi Mvurya ni hatua kubwa iliyopigwa katika demokrasia na hasa katika kuwapa wanawake nafasi ya uongozi.

Huku hayo yakijili huko Nairobi, wanafunzi wa chuo cha TUM waliwanyima maafisa wa kupambana na ghasia nafasi ya kucheza mchezo wa paka na panya.

Hii ni kufuatia utulivu wa ajabu uliotawala baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa mnamo Aprili 5.

Katika adhuhuri hiyo yenye jua kali, wanafunzi waliojawa na msisimko wa aina yake walishinda wakikimbia chuoni huku na kule, huku wakiimba nyimbo za ushindi na sherehe.

Dennis Okang’a, kiongozi mpya wa wanafunzi chuoni TUM akihutubu baada ya ushindi. Picha/ Steve Mokaya

Inaonekana kuwa hali hii ilileta hofu kwa uongozi wa chuo hicho, na hivyo basi wakaagiza maafisa wa usalama ili kutuliza machafuko-tarajiwa.

Hata biashara zilizoko chuoni humo na karibu na chuo hicho zilifungwa kwa muda, wafanyabiashara wakiohofia usalama wao.

Ila matokeo yalipotangazwa, wanafunzi wenye bashasha walijaa barabarani huku wakiimba na viongozi waliokuwa wamechagukiwa.

Polisi wengi waliokuwa wamepiga kambi nje ya lango kuu walitizama kwa mshangao, wasijue la kufanya.