Habari Mseto

Mwanamume afariki kwa kuzidiwa na mahanjamu

August 13th, 2019 1 min read

Na WYCLIFFE KIPSANG na CECIL ODONGO

WAKAZI wa lokesheni ya Ngeria, Kaunti ya Uasin Gishu wameamkia habari za kusikitisha za mwanamume aliyefariki katika hali ya kutatanisha baada ya kushiriki ngono na mjane mwenye umri wa miaka 50.

Mwanamume huyo alikumbana na kifo akiwa na umri wa miaka 35.

Inadaiwa alikuwa akinywa pombe kwenye baa moja eneo la Sachangwan karibu na uwanja wa ndege wa Eldoret Jumapili usiku, alipokutana na mwanamke huyo ambaye jina lake bado halijabainika.

Wakazi walikuwa wakiendelea kumiminika katika shamba la mahindi kutazama mwili wa mwanamume huyo ambaye mauti yalimpata akila uroda na mwanamke huyo shambani humo.

Mwanamke huyo aliwasimulia polisi jinsi mpenzi wake alizidiwa na mahanjamu baada ya kumeza vidonge vya kusisimua mwili kimapenzi.

Chifu wa kata ya Ngeria Mathew Arusei aliwatahadharisha vijana dhidi ya kujihusisha na masuala yasiyo ya kimaadili kama kushiriki ngono na kunywa pombe kiholela.

Polisi kutoka kituo cha Kiambaa waliowasili kwenye eneo la tukio walichukua mwili wa mwendazake na kuupeleka katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH).