Habari

Mwanamume afariki Magongo katika mkasa unaokisiwa ni hitilafu katika nyaya za stima

December 3rd, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

MWANAMUME aliyekuwa na umri wa miaka 34 kutoka Magongo kwa Hola mjini Mombasa amefariki baada ya kupigwa shoti ya stima.

Akithibitisha tukio hilo kamanda wa polisi wa eneobunge la Changamwe Issa Mahmoud alisema marehemu Oscar Nyange alipigwa shoti na nyaya za kupitisha stima zilizokuwa zimekatika.

“Muunganisho wa nyaya za stima katika chumba chake tunakisia ulikuwa na hitilafu. Hata hivyo, bado tunachunguza kujua chanzo cha shoti hiyo,” akasema Bw Mahmoud.

Marehemu ambaye alikuwa anaishi peke yake katika nyumba ya kulipia kodi anadhaniwa kuwa alikanyaga waya wa stima alipokuwa anajitayarisha mapema jana Jumatatu kuelekea kazini.

Usiyahi

Kulingana na jirani ya marehemu Bi Fatuma Shomar, alipokuwa anaendelea na shughuli zake, alisikia unyende kutoka kwa chumba cha marehemu.

Hata hivyo, juhudi zao za kumuokoa hazikufua dafu kwani walipoingia katika chumba hicho tayari Bw Nyange alikuwa ameaga dunia.

“Hatujui nini kilitokea. Tulisikia kelele lakini kufika tukamkuta marehemu ameanguka chini. Tulipojaribu kumpatia huduma ya kwanza tulitambua kuwa tayari alikuwa ashaaga dunia,” Bi Shomar alieleza.

Alirudia kusema Nyange alikuwa anaishi pekee katika chumba hicho.

Alielekezea lawama kampuni ya kusambaza umeme nchini kwa kutochunguza jinsi nyaya za stima zinavyounganishwa mashinani.

Ameitaka kampuni hiyo iwe ya kushughulikia nyanya zilizo na tashwishi mara wanapofahamishwa na wakazi ili usalama uwepo.