Habari Mseto

Mwanamume ajitahiri kwa wembe ili kuepuka kejeli za mke

January 14th, 2019 2 min read

Na ALEX NJERU

MWANAMUME wa miaka 40 kutoka eneo la Ntulili, Maara, Kaunti ya Tharaka-Nithi, Jumapili alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Chuka baada ya kujitahiri.

Afisa mkuu wa polisi wilaya hiyo, Bw Johnston Kabusia, aliiambia wanahabari kwamba mwanamume huyo, ambaye ni baba ya watoto watatu, alipatikana na mkewe ndani ya nyumba akivuja damu nyingi kwenye uume wake, na ndipo akawaita wanaume wa kijiji ambao walimkimbiza hospitalini.

Bw Kabusia alisema matukio yaliyopelekea kisa hicho yalianza mkewe alipowajulisha wanaume wa kijiji kwamba mumewe hakuwa ametahiriwa kulingana na mila za jamii ya Ameru.

“Siku ya Jumamosi watu wapatao 100 walifika nyumbani kwa bwana huyo ili kuthibitisha habari hiyo, lakini alifanikiwa kutorokea kwenye misitu ulio karibu. Kwa mujibu wa ripoti niliyopata, mtu huyo alijitahiri kwa kutumia wembe lakini hakujitengeneza vizuri kwani alijiumiza sana,” alisema Bw Kabusia.

Alieleza kuwa polisi wanachunguza ili kuthibitisha hasa kilichotokea.

Daktari mkuu wa hospitali ya Chuka, Bi Maurine Ogeto alisema mwanamume huyo alitibiwa vizuri na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Madaktari waliweza kumtibu na kumtengeneza vizuri ili kuhakikisha kuwa kila kitu kilikuwa sawa na akaruhusiwa kwenda nyumbani,” alisema Dkt Ogeto.

Jirani ya mwanamume huyo alisema aliishi mbali na nyumbani wakati wa ujana wake, lakini akarudi nyumbani akiwa mtu mzima na ndio sababu hakuna mtu angejua kwamba hakuwa ametahiri.

“Tumekuwa tukijua kwamba ametahiri hadi wakati mke wake alipotoboa siri,” alisema jirani huyo.

Katika hospitali hiyo hiyo, mwanamume mwingine kutoka eneo la Mariani wilaya ya Chuka/ Igambang’ombe anaendelea kupata matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa pete iliyokwama kwenye sehemu yake ya siri.

Kwa mujibu wa daktari, mwathiriwa huyo alifikishwa hospitalini Jumamosi baada ya kushindwa kutoa pete ambayo ilikuwa tayari imefanya sehemu yake ya siri kufura.

Alisema mwamume huyo alipelekwa kwenye chumba cha upasuaji na akadungwa dawa za usingizi kabla ya pete hiyo kutolewa.

“Mwanamume huyo alikuwa amefura sana kwenye sehemu yake ya uume na ilikuwa imeumia sana alipokuwa akijaribu kuitoa kwa nguvu,” alisema daktari.