Afya na Jamii

Mwanamume akejeliwa kwa kuruhusu mkewe kupanga uzazi

March 28th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

WAVUMISHAJI wa afya ya jamii katika wadi za Heilu na Manyatta zilizoko mjini Moyale, Kaunti ya Marsabit, wanazidi kupata pingamizi katika juhudi zao za kueneza ujumbe wa umuhimu wa upangaji uzazi.

Hali hii inasababishwa na misimamo ya wanajamii kutokana na mafundisho ya kidini, utamaduni wao na pia wanasiasa kuwahimiza kuzaana ili maeneo yao yawe na wingi wa watu.

Data kutoka hospitali ya Kaunti ndogo ya Moyale zinaonyesha kuwa kata ya Heilu iliyo na wanawake 6,800, ni wanawake 22 ambao wanapanga uzazi.

Kati ya 22, wawili pekee ndio wameruhusiwa na waume wao.

Kilomita tano kutoka mjini Moyale hadi katika kijiji cha Heilu, mhudumu wa afya ya jamii Bw Abdi Gadallo, anavumilia kejeli kutoka kwa wenzake baada ya kuruhusu mkewe kupanga uzazi.

Baba huyo wa watoto wanne, aliambia Taifa Leo kwamba alitaka kuwa kielelezo bora kwa jamii na kuondoa dhana mbovu ya upangaji uzazi.

“Kwa kuhimiza mke wangu kupanga uzazi, nilitaka kufahamisha jamii bado unaweza kupata mtoto mwingine katika siku za usoni. Watoto wana umri wa kati ya miaka 14, minane, mitano na mitatu  baada ya mimi na mke wangu kupanga uzazi. Lakini pingamizi zipo. Pia, kudharauliwa na jamii kwamba hatua yetu ni kichekesho,” akasema Bw Gadallo mnamo Jumatano.

“Kuna ushidani kutoka kwa wanasiasa. Hapa tuna jamii zaidi ya tatu na kila kiongozi anataka kabila au ukoo wake uwe na watu wengi ambao watamchagua. Hivyo anahimiza wakazi waweze kuzaa bila mapumziko ili idadi ya watu isipungue miaka 10 ijayo,” akasema.

Mhudumu huyo wa afya alisema visa vya wanawake kupewa talaka vimeongezeka katika eneo hilo.

 

Mji wa Moyale, ambapo visa vya wanawake kupewa talaka vinaripotiwa kuongezeka kwa sababu ya kutumia mbinu za upangaji uzazi. PICHA | FRIDAH OKACHI

Hii ni baada ya waume kuwa na dhana ya kuwa wake wao huenda pengine wanatumia mbinu ya upangaji uzazi bila kuwajulisha.

“Mzee akikaa na mkewe kwa mwaka mmoja bila kupata mtoto, anampa mke huyo talaka. Visa hivi vimeongezeka sana,” alisikitika mvumishaji huyo wa afya ya jamii.

Kilomita tatu kutoka kwa mhudumu huyo, Taifa Leo ilimtembelea Bi Fatuma Abdi nyumbani kwake. Yeye ni mama wa watoto wawili. Anasema alitengwa na jamii kwa kutumia mbinu za upangaji uzazi.

Bi Abdi anasema ni miaka mitatu tangu aanze kutumia mbinu ya upangaji uzazi, Anasema hiyo kwake ni hatua nzuri japo imechukuliwa visivyo na jamii.

“Niliweka mwaka 2021 lakini nanyanyapaliwa na marafiki. Nina upweke kwa kuwa siwezi kutangamana na wanawake wenzangu wenye mtazamo tofauti kuhusu suala hili kama hapo awali,” akasema Bi Abdi.

Hali hiyo imesababisha mumewe aliyepania kupata watoto watatu pekee kumshauri asiitumie tena mbinu hiyo mara atakapoitoa.

“Unyanyapaa umesababisha mzee wangu kusema wakati muda wake wa kutolewa ukifika, nisiweke kitufe kingine cha upangaji uzazi,” akasema.