Habari Mseto

Mwanamume akiri kutapeli watu kwa miaka mitatu akijifanya kuwa mume wa hakimu

January 31st, 2024 2 min read


NA MAUREEN ONGALA

MWANAUME anayehudumu katika shule moja ya kibanfsi eneo la Kiamaiko, Nairobi, amekiri kuwa alijifanya kuwa mpenzi wa Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Mahakama ya Kilifi, Bi Ivy Wasike kwa miaka mitatu.

Cryspinus Malenya Inyama, 29, kutoka Khayega, Kaunti ya Kakamega, alikiri makosa hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kilifi, Bw Daniel Sitati ambapo alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kutapeli watu na pia kujifanya kuwa mumewe hakimu Wasike.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini, Inyama amekuwa akiwalaghai pesa wafanyakazi wenza wa hakimu Wasike, marafiki na pia wanafamilia kwa kudai kutumiwa hela za chakula cha mchana, zawadi na hata pesa za kwenda kuvinjari.

Kulingana na hakimu Wasike, alinunua laini mpya ya Safaricom kati ya mwaka wa 2010 na 2011 na akaanza kuitumia rasmi kama yake.

Lakini mapema 2020 aligundua ya kwamba laini hiyo ilikuwa inatumika na mtu mwingine kwani alikuwa anapokea simu kutoka kwa watu wake wa karibu kuwa walikuwa wamezungumza kupitia njia ya SMS, mambo ambayo hakuelewa.

Aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kilifi OB/31/09/01/2024.

Bi Wasike alisema kuwa pia aliripoti kwa kitengo cha kuwahudumia wateja cha kampuni ya Safaricom mara tatu bila mafanikio. Aliambiwa kuwa lilikuwa jukumu lake kuwajulisha watu wake kuwa alikuwa hatumii laini hiyo tena.

“Safaricom waliniambia kuwa laini hiyo ilikuwa imepewa mtu mwingine kwa hivyo niwafahimishe watu wangu kuwa situmii laini hiyo tena,” akasema Bi Wasike.

Ingawa alinunua laini nyingine, ilikuwa changamoto kwake kupigia kila mmoja na kumfahamisha kuwa laini yake wanayojua ilikuwa haitumiki tena.

“Watu waliokuwa wananipigia simu waliniuliza jinsi mpenzi wangu anavyojibeba wakati anapochukua simu zake na kuwa alikuwa anawauliza maswali ya kushangaza akiitisha kufanyiwa mambo, pesa ya lanchi, na pia za kwenda kuvinjari wikendi,”akasema.

Hakimu Wasike alisema mshtakiwa alikuwa na orodha yote ya majina katika simu yake na aliwapigia simu ama kutuma jumbe kwa WhatsApp akidai kuwa alikuwa yeye.

“Hali hii iliniharibia jina na jinsi majaji, wafanyakazi wenzangu na marafiki walivyonichukulia kwa staha kila mara tulipokutana katika mikutano ya kikazi ama sherehe.

“Walishinda kuniuliza ni mwanaume aina gani ambaye niko naye kwa jinsi alivyojibeba hasa kwa wenzangu wa kike,” akasema.

Jana Inyama alishtakiwa kumtapeli Dkt Vincent Chokaa ambaye ni wakili katika Mahakama ya Juu jijini Nairobi na Mombasa Sh2,000.

Hii ni baada ya kumtumia ujumbe kwa WhatsApp akijifanya kuwa Bi Wasike na kuomba New Year.

Dkt Chokaa alimwambia ampe muda ajipange lakini hapo kwa hapo mshtakiwa alimuliza Bw Chokaa iwapo angetuma pesa hizo.
Wakili akatuma Sh2,000 kwa laini halali ya Bi Wasike.

Mshtakiwa alisema aliponunua laini hiyo mwaka 2020, alianza kupigiwa simu kutoka kwa watu wakimtafuta Ivy.

Ndipo alipogundua ya kwamba anayetafutwa kwa simu ni mtu muhimu.

Alisema licha ya kuwakataza wanaopiga simu kuwa hakuwa hakimu Wasike, walishinda kumpigia simu na kumtumia jumbe.

Maafisa wa upelezi kutoka Kilifi walimkamata Bw Inyama Januari 15 na kumfikisha mahakani Kilifi ambapo walipewa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi wao.

Hakimu Sitati aliagiza kiongozi wa mashataka kuwakilisha ripoti kabla ya mahakama kutoa hukumu.

Mshtakiwa atafikishwa kortini Februari 13 kusomea kifungu.