Kimataifa

Mwanamume akiri kuwaua wagonjwa 100 kwa sumu

November 1st, 2018 2 min read

MASHIRIKA NA PETER MBURU

MWANAMUME aliyekuwa muuguzi nchini Ujerumani amekiri mbele ya korti kuwa aliwaua wagonjwa 100 kwa kuwapa dawa zenye sumu ili kuwapa mshtuko wa moyo, katika hospitali mbili kaskazini mwa taifa hilo.

Wapelelezi walisema kuwa Bw Niels Hogel alifanya vitendo hivyo kwa nia ya kuwaridhisha wafanyakazi wenzake, kwa kuwarejesha uhai baada ya kuwavamia.

Hadi sasa, Bw Hogel mwenye umri wa miaka 41 anahudumia kifungo cha maisha kwa kusababisha vifo sita alipokuwa muuguzi.

Anasemekana kuwaua wagonjwa 36 alipokuwa katika mhospitali ya Oldenburg na 64 katika hospitali ya Delmenhorst kati ya 1999 na 2005.

Alipoulizwa na jaji katika mahakama ya Oldenburg ikiwa mashtaka hayo yalikuwa ya kweli, mshukiwa alisema kuwa yote yalikuwa kweli.

Makumi ya watu wa familia za wagonjwa waliofariki mikononi mwa mshukiwa walikuwa kortini kumsikia akikiri, wengine wakitaka kufahamu namna alifanikiw kutekeleza mauaji mengi kiasi hicho katika hospitali mbili.

Inasemekana kuwa hata baada ya kupatikana moja kwa moja akiteleza moja kati ya mauaji hayo, Hogel aliruhusiwa kufanya kazi kwa siku mbili zaidi, ambazo bado alimuua mgonjwa mwingine.

Wanafamilia wengi wanaamini kuwa hospitali hizo ziliamua kunyamazisha habari kuhusu mauaji hayo.

Uchunguzi unaendeshwa kubaini ikiwa hatua ya hospitali hizo ilichangia kukuza ndoto ya mmoja wa watu wauaji zaidi nchini Germany, tangu vita vya vili vya dunia.

Msemaji wa familia hizo Christian Marbach alisema kuwa hiyo ilikuwa sakata kubwa kwani wasimamizi wa hospitali hizo walimpa fursa muuguzi huyo kuua bila kuingilia kati.

“Tulipigania sana ili Hogel ashtakiwe na tunatarajia kuwa atahukumiwa kwa mauaji mengine 100,” akasema Bw Marbach, ambaye babu yake aliuawa na mshukiwa huyo.

Hogel alipatikana kwa mara ya kwanza 2005 akimdunga mgonjwa dawa ambayo haikuwa imeshauriwa na daktari katika hospitali ya Delmenhorst. Mnamo 2008 alifungwa miaka saba kwa kujaribu kuua.

Miaka ya 2014 na 2015, mwanaume huyo alipatikana na hatia ya mauaji ya wagonjwa wawili, na mawili ya kujaribu kuua wagonjwa na akafungwa maisha.

Wakati wa kesi hizo, alikiri mbele ya korti kuwa alikuwa ameua watu 30. Hii iliwapelekea wachunguzi kufukua mili takriban 130 ambao waliwahi kuaga dunia katika mikono yake, ili kubaini dawa ambazo huenda ziliwapelekea kupata mishtuko ya moyo.

Rekodi katika hospitalli ya Oldenburg ambapo alifanya kazi zilionyesha kuwa visa vya vifo, na majaribio ya kuwafufua watu viliongezeka maradufu wakati Hogel alikuwa kazini.