Habari Mseto

Mwanamume akosa raha ya ndoa kugundua watoto wote 5 si wake

February 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME Mkenya kwa jina Ombaso amevunjwa moyo na barafu ya moyo wake, baada ya kugundua kuwa mkewe wa miaka kumi ameishi kusaliti penzi lao.

Kulingana na mwanamume huyo ambaye sasa anaishi kwa huzuni na bila matumaini, walikosana na mkewe kiwango cha kumfanya kurejea nyumbani kwa wazazi wake.

Hata hivyo, alipokuwa nyumbani kwao, mama mkwewe alimpigia simu na kumpa maneno yaliyomwacha kupigwa na butwaa.

Mama huyo alimfahamisha kuwa watoto wote watano ambao walikuwa nao pamoja na mkewe na ambao wamewalea pamoja muda wote walipokuwa katika ndoa hawakuwa wake.

Baada ya hapo mkewe aliondoka maishani mwake na kwenda kumzalia mwanamume mwingine watoto.

Hii ni licha ya kuwa Bw Ombaso amekuwa akiwalea watoto hao kama wake mwenyewe.

Mwanamume huyo alitoboa haya kupitia stesheni moja ya redio humu nchini mnamo Januari 22, ambapo alisema alijaribu kila juhudi kupigania penzi la mwanamke huyo tena lakini akashindwa.

“Wakati tulipozozana, mke wangu aliondoka na kwenda nyumbani kwa wazazi wake. Mamake baadaye alinipigia na kunijulisha kuwa hakuna mtoto yeyote kati ya watano tuliokuwa nao ni wangu,” akasema Bw Ombaso.

Alisema maneno hayo yalimfanya kutafuta huduma za kupima DNA, ambapo alidhibitisha kuwa ni kweli watoto hao si wake.