Habari Mseto

Mwanamume aliyedai mkewe alijitoa uhai yabainika alimuua


MWANAMUME amepatikana na hatia ya mauaji baada ya kubainika kuwa, alimuua mkewe na kufanya eneo la mkasa kuonekana kama mwanamke huyo alijitoa uhai.

Mutua Mwanzia sasa huenda akafungwa jela kwa muda mrefu baada ya Mahakama Kuu ya Mombasa kumpata na hatia ya kumuua Mary Wanjiku Waweru.

Jaji Anne Ong’injo alisema ingawa hakuna mtu aliyeona marehemu akiuawa, Mwanzia ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana naye na hakufafanua alikuwa wapi wakati kisa hicho kilipotokea.

Jaji alibaini kuwa chembechembe za dawa ya kuua wadudu na matumizi ya waya kumfunga marehemu kwenye grili ya dirisha ili aonekane kama alijiua kwa kujinyonga ni ushahidi wa uovu aliokuwa nao mshukiwa.

Jaji Ong’injo alisema kuwepo kwa chembe za sumu katika sampuli zilizochambuliwa na Maabara ya Serikali na jinsi marehemu alivyopatikana katika eneo la tukio, kunaifanya mahakama yake kuamini kuwa kifo kilisababishwa na mtu.

“Kwa kumalizia, mahakama hii imeona kwamba upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote. Mtuhumiwa amepatikana na hatia ya kosa la mauaji,” alisema jaji.

Alifariki kwa kubanwa shingo

Pia, Jaji huyo alibainisha kuwa ingawa madaktari wa upasuaji walikuwa na maoni kuwa marehemu alifariki kwa kubanwa shingo na kukosa hewa kutokana na kunyongwa, mahakama iliangalia picha za marehemu, na kubaini kuwa haiwezekani kiuhalisia mtu anaweza kufa kwa kunyongwa kwenye sehemu ambayo urefu wake ni chini sana kuliko urefu wa mwili.

“Haina maana kwamba marehemu angemeza sumu kisha kujinyonga,” akaongeza.

Picha hizo zilimuonyesha marehemu akiwa amefungwa kwenye sehemu ya chini kabisa ya dirisha la chumba chao cha kulala huku akiwa amejiinamia kitandani miguu ikiwa chini.

Mwanzia alikana kumuua mkewe. Hati ya mashtaka inaonyesha alitenda kosa hilo mnamo Mei 13, 2016 katika eneo la Ushindi, Kaunti Ndogo ya Likoni, Mombasa.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi 16 wakiwemo watoto wa marehemu kuunga mkono kesi yake kwamba Mwanzia alitenda kosa hilo.

Watoto hao waliambia mahakama kuwa wazazi wao walikuwa wakizozana na kupigana mbele yao.

“Baba yetu angempiga mama yetu. Siku hiyo mama aliniaga na kurudi sebuleni kulala huku nikielekea shuleni asubuhi. Baadaye niliambiwa mama yangu amefariki,” alisema mtoto mwenye umri wa miaka minane.

Dadake mwenye umri wa miaka 13 pia alithibitisha kuwa wazazi wao walikuwa wakipigana sana.

“Lakini siku hiyo sikuwasikia wakipigana. Niliwaacha na dada yangu nilipokuwa nikienda shuleni asubuhi. Baadaye niliambiwa mama yetu amefariki,” alisema.

Aseama kifo chake kilimshtua

Akijitetea, Mwanzia alikana kumuua mwanamke huyo lakini alieleza kuwa kifo chake kilimshtua kwa sababu alikuwa amemuacha nyumbani akienda kazini.

Alisema walikuwa wanafanya biashara ya M-Pesa, kinyozi na ya kutengeneza sharubati na kwamba walitofautiana kuhusu hesabu za fedha katika biashara ya M-Pesa haikuwa inalingana.

“Nilimwambia marehemu kwamba tutazungumza juu ya suala hilo baada ya kazi kwani shida ya hesabu za pesa kutolingana katika biashara hiyo ya M-Pesa ulikuwa wa mara kwa mara,” alisema.

Mwanzia aliambia mahakama kuwa mkewe alikuwa na hasira. Alimweleza atalazimika kumwajiri mtu mwingine lakini marehemu alimwambia kuwa alitaka kumpeleka mpango wake wa kando kwenye duka hilo.

Mshtakiwa pia alisema mwaka 2008, marehemu alijaribu kujitoa uhai kwa kutumia dawa kupita kiasi huku akimtuhumu kuwa alionekana akiwa na mwanamke mwingine mjini.

“Alipelekwa katika zahanati ambapo huduma ya kwanza ilitolewa na akapona. Alihojiwa na daktari na kushauriwa,” alisema.
Mshtakiwa pia alisema kuwa mkewe alikuwa na hasira na angeweza kufanya chochote bila kufikiria.