Mwanamume aliyedaiwa kujifanya hakimu ashtakiwa

Mwanamume aliyedaiwa kujifanya hakimu ashtakiwa

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME aliyekamatwa Nakuru kwa kujifanya hakimu, jana alishtakiwa katika mahakama ya Eldoret kwa kujipatia zaidi ya Sh 1 milioni kwa ulaghai kutoka kwa mfanyabiashara wa Eldoret, alijidai angemsaidia kupata nafasi za ajira katika mahakama ya Nakuru na kwa kampuni ya Kenya Pipeline.

Victor Kiprono Ng’eno ambaye alikamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha Upelelezi wa Jinai DCI mjini Nakuru Oktoba 9, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan.

Mahakama iliambiwa siku tofauti kati ya Oktoba 1, 2019 na Januari 6, 2020 katika mji wa Eldoret, alijipatia Sh 1,022,972 kutoka kwa Joyce Chepchirchir Ng’etich akijifanya kuwa hakimu wa mahakama ya Nakuru.

Alidai alikuwa na uwezo wa kumsaidia kupata kazi katika idara ya Mahakama na kampuni ya Kenya Pipeline.Hata hivyo mshtakiwa alikana mashtaka hayo huku akiomb akuachiliwa kwa dhamana.Ombi lake la kuachiliwa kwa bondi lilizimwa na upande wa mashtaka ukibaini kuwa alikuwa na kesi sawa na hiyo katika mahakama ya Nakuru ambapo alinyimwa bondi hivyo basi kulikuwa na sababu tosha ya mahakama ya Eldoret kumnyima bondi.

Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuwaruhusu kupitia faili yake ya Nakuru ili kubaini msingi wa kunyimwa dhamana katika kesi nyingine ya mashtaka sawa inayomkabili mahakamani Nakuru.’Tunapinga kuachiliwa kwake kwa dhamana kwa kuwa ana kesi kama hiyo mjini Nakuru na alinyimwa dhamana.

Turuhusu tupitie faili ya Nakuru ili kubaini sababu zilizofanya mahakama kumnyimwa dhamana katika mahakama ya Nakuru,” upande wa mashtaka uliambia mahakama.Mshtakiwa alipinga ombi la upande wa mashtaka la kumnyima bondi.

Aliiambia mahakama kuwa alikuwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo hivyo hali yake imeendelea kudorora kaitka rumande.Mahakama itatoa uamuzi wa kuachiliwa kwa dhamana siku ya Ijumaa (leo).

Alipokamatwa mjini Nakuru maafisa wa upelelezi walikuwa wameeleza kuwa hakimu huyo ghushi pia alikuwa akijifanya nduguye Waziri wa Ugatuzi Charles Keter.Mmoja wa waathiriwa wake wa Nakuru aliyetambulika kama Samuel Soi alifichua kuwa huku akijifanya kakake waziri Keter, alimlaghai Shilingi 1.6 Milioni kwa ahadi ya kumtafutia kazi.

Mwathiriwa mwingine pia alifichua kuwa mshtakiwa alimlaghai Sh100,000 kwa ahadi ya kuharakisha kesi yake katika mahakama ya Nakuru.Makosa hayo ya Nakuru yanadaiwa kutokea kati ya Machi 15, 2018 na Desemba 31, 2019.Kesi yake Nakuru itasikizwa Novemba 2.

You can share this post!

Polo ajifanya sonko kumbe kijijini ni hoi

Walioteketeza shule watozwa Sh50,000

T L