Makala

Mwanamume aliyefungwa jela miaka 30 aomba korti impe mkewe Sh100,000

February 3rd, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA meneja wa kampuni ya usafirishaji mizigo kwa ndege ya Uholanzi iliyokuwa na ofisi zake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kumuua afisa wa jeshi (KDF).

Richard Mwangi Mugo alisukumwa gerezani na Jaji Daniel Ogembo mnamo Ijumaa baada ya kutupilia mbali ombi lake ahukumiwe kifungo cha nje kwa vile yuko na watoto wadogo wanaomtegemea na mke.

“Ijapokuwa umekana ulimuua John Machimbo Litala,55, usiku wa Desemba 3, 2018, katika eneo la Njiru, hii mahakama imekupata na hatia kwa miale ya simu yako ambayo inaonyesha ulikuwa pahala pa mauaji ya marehemu saa kumi na moja alfajiri,” Jaji Ogembo alisema.

Jaji huyo alisema mbali na kuwa hapo, alijiwekea pesa kupitia kwa M-Pesa kutoka kwa simu ya marehemu.

Licha ya kukataa katakata kwamba alimuua Machimbo, Jaji Ogembo alisema utawazi wa kampuni ya Safaricom hauwezi mwekelea uwongo , eti alikuwa katika eneo la Kiathieko iliyoko9 eneo la Ruai Lokesheni ya Njiru saa 11 na dakika tisa na sekunde mbili Desemba 3,2018.

Na wakati huo huo Jaji Ogembo alisema miale ya simu ya Mugo nambari 0721773170 na ile ya marehemu 0711800665 ilionyesha walikuwa pamoja hapo Kiathieko saa hiyo 5.09.02 alfajiri.

Jaji huyo alikubaliana na  ushahidi wa afisa wa polisi Benjamin Mumo aliyechunguza hiyo kwamba “Ni Mugo tu aliyekuwa mahala Machimbo aliuawa.”

Akitoa adhabu Jaji Ogembo alisema Mugo hastahili huruma hata!

“Mshtakiwa hastahili huruma kwa vile walimtesa Machimbo sana wakimshurutisha awaambia namba yake ya siri ya mtandao wake wa MPesa. Walimpiga na kumfunga mikono na miguu kumshurutisha afichue namba ya siri ya MPesa,” Jaji Ogembo alisema.

Mbali na kumtesa vile walimnyonga wakitumia shuka aliyokuwa amebeba ya Maasai.

Hatimaye walifunika maiti yake nayo.

Wapitanjia waliuona mwili wa Machimbo na kuwapasha habari polisi waliopata kitambulisho chake cha KDF, kitambulisho chake cha uraia na kadi za benki.

Pia walitoa cheti cha malipo cha Novemba 2018.

Washambuliaji wake walitumia ukanda wenye maandishi ya KDF kumfungia mikono mgongoni.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Bi Mercy Njoroge uliwaita mashahidi 10 ambao jaji Ogembo alisema walithibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa.

Mahakama ilisema ni mshtakiwa tu na majambazi wenzake waliomuua Machimbo.

“Unastahili adhabu kali. Hustahili kuhurumiwa kamwe. Ushahidi wako kwamba usiku huo wa Desemba 3, 2018, ulinyang’anywa simu ukitoka Zimmerman katika michezo ya vishale hauna mbele wala nyuma. Hauna mashiko kamwe kisheria,” alisema jaji Ogembo.

Jaji alisema Mugo alidanganya ilimchukua siku saba kununua laini nyingine ya simu baada ya kudai aliibiwa simu usiku wa Desemba 2/3, 2018, lakini aliinunua keshoye kulingana na ushahidi wa mkewe, Bi Margaret Wangare.

Mahakama ilisema mshtakiwa alitofautiana kabisa na ushahidi wa mkewe kuhusu simu iliyopotea na matukio ya Jumapili ya Desemba 2, 2018.

Mugo alisema alitoka kazini na kupata mkewe akiwa ameenda Kanisani mnamo Desemba 2, 2018, lakini mkewe aliambia mahakama alimwacha mumewe akitazama runinga akienda kwa maombi pamoja na watoto.

Hawakumpata Mugo kwa nyumba wakitoka kanisa na kwamba alirudi alfajiri akiwa ananuka pombe na nguo zake zikiwa chafu.

Mugo alidai alianguka nguo zake zikapata uchafu.

“Ushahidi wako na mkeo unatofautiana sana. Pia madai ulikuwa unashikiriki mchezo wa mishale Zimmerman haufui dafu kwa vile hukuita hata mchezaji mmoja kuthibitisha ulikuwa Zimmerman,” alisema Jaji Ogembo.

Mahakama ilitupilia mbali ushahidi wote wa mshtakiwa ikisema “ni uzushi tu ndiye alimuua Machimbo.”

Wakili wake, bW Gordon Ogada, alipinga ushahidi wa Safaricom uliothibitisha Mugo alikuwa pahala pa mauaji akidai polisi hawakuambatanisha na cheti jinsi inavyotakiwa kisheria.

Jaji Ogembo alitupilia mbali ombi hilo akisema Bw Ogada alichelewa kuwasilisha ombi lake awali lakini akaleta kesi ikiamuliwa.

Mkewe Machimbo alieleza mahakama kwamba mauaji ya mumewe yalimsababishia ugonjwa wa moyo na anaomba familia ya mfungwa igharimie matibabu yake.

Baada ya kuhukumiwa, Mugo aliomba mahakama imrudishie mkewe dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 ikimu mahitaji ya watoto.