Habari Mseto

Mwanamume aliyejifanya mwanamke abambwa

March 13th, 2019 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

POLISI Kaunti ya Lamu wanamzuilia mwanamume wa makamo kwa kujifanya kuwa mwanamke.

Akithibitisha tukio hilo Jumatano, Kamanda wa polisi wa kaunti ya Lamu Muchangi Kioi, alisema mwanamume huyo wa umri wa miaka 22 alitiwa mbaroni katika mtaa wa Kashmir mjini Lamu.

Alikuwa amevaa buibui na kujirembesha kwa vipodozi huku akitembea kama mwanamke.

Bw Kioi alisema mshukiwa anazuiliwa kwenye kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi ili kubaini kiini cha tabia yake.

“Ni kweli. Maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria eneo la Kashmir walimpata jamaa huyo akiwa amevalia nguo za kike, ikiwemo buibui na kujirembesha kwa vipodozi. Alikuwa akitembea kama mwanamke na hata kuongea kwake kulikuwa kwa jinsi ya kike. Uchunguzi tayari unaendelea ili kubaini sababu ya mshukiwa kujifanya mwanamke,” akasema Bw Kioi.

Si mara ya kwanza kwa polisi eneo la Lamu kuwakamata washukiwa wakiwa katika halio tatanishi.

Mnamo Septemba, 2018, mwanamume wa umri wa makamo alikamatwa kwenye makazi ya madakari na wauguzi katika hospitali ya King Fahad mjini Lamu ilhali akiwa na vifaa vya kutebngenezea bomu na vilipuzi.

Mnamo Januari mwaka huu, polisi eneo la Kiunga kwenye mpaka wa Lamu na Somalia walimkamata mwanamume wa miaka 37 kwa kujifanya kuwa afisa wa ujasusi katika kitengo cha jeshi la Kenya (DMI).