Kimataifa

Mwanamume amnyonga simba hadi kufa

February 11th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MAAFISA wa sekta ya uhifadhi wa wanyama pori wamesema kuwa mwanamume kutoka eneo la kaskazini mwa Colorado, Marekani alimuua simba kwa kumnyonga, wakati mnyama huyo alimvamia.

Iliripotiwa kuwa mwanamume huyo alikuwa akitoroka akiwa peke yake karibu na makavazi ya Fort Collins wakati alivamiwa na simba kutoka nyuma.

Msemaji wa mbuga ya Colorado Rebecca Ferrell alisema kuwa mwanamume huyo alifahamisha wachunguzi kuwa alimnyonga simba huyo hadi kufa, jambo ambalo lilithibitishwa na ripoti ya upasuaji wa mzoga wa samba huyo.

Ferrell alisema kuwa mwanamume huyo alifanya vyema kwa kupigana na mnyama huyo kujitetea kadri ya uwezo wake.

Kwa kuwa alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia, hakuwa na silaha yoyote na hivyo ilimbidi kujitetea kwa mikono tu.

Baada ya vita vikali na kumuua mnyama huyo hatari, aliruka ua na kujiendesha hadi hospitalini kwani alikuwa amejeruhiwa usoni, mikononi, miguuni na mgongoni.

Baada ya kisa hicho cha Jumatatu, Jumanne usimamizi wa mbuga ya Colorado ulithibitisha maelezo yake kuwa alimuua mnyama huyo kwa kumnyonga.

Mavamizi ya simba dhidi ya watu wanaozuru milima huwa hayashuhudiwi sana, kwani tangu 1990 ni watu 16 pekee ambao wamevamiwa na wanyama hao, nao watatu wakauawa.