Habari Mseto

Mwanamume anayedaiwa kumuua bintiye akamatwa

March 26th, 2024 1 min read

MAAFISA wa polisi katika eneo la Navakholo, Kaunti ya Kakamega, wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 32 anayedaiwa kumuua bintiye na kuutupa mwili wake barabarani.

Bw James Wafula kutoka kijiji cha Kochwa, Sidikho, aliripotiwa kuzozana na mke wake Bi Florence Wafula mnamo Jumatatu usiku, kabla ya kumgonga mtoto mwenye umri wa miaka tisa kwa kifaa butu na kumuua papo hapo.

Polisi walisema kwamba baada ya kutekeleza unyama huo, mshukiwa aliutupa mwili wa binti yake barabarani, mita chache kutoka nyumbani kwao.

Majirani walipata mwili huo Jumatatu asubuhi.

Kamanda wa Polisi Navakholo, Bw Richard Omanga, alisema mwili wa mtoto ulikuwa na majeraha kichwani na usoni.

“Mwili ulikuwa unatoka povu mdomoni na damu kutiririka kupitia masikio na puani, ishara kuwa uligongwa kwa kifaa butu kilichosababisha majeraha ya ndani,” alisema Bw Omanga.