Mwanamume anayehusishwa na genge la ‘Jeshi ya Gaica’ atozwa faini ya Sh30,000 kwa makosa matatu

Mwanamume anayehusishwa na genge la ‘Jeshi ya Gaica’ atozwa faini ya Sh30,000 kwa makosa matatu

Na MWANGI MUIRURI

MWANAMUME ambaye inadaiwa ni mkuu wa genge linalojiita ‘Jeshi ya Gaica’ katika Kaunti ya Murang’a, akiwa mshukiwa wa makosa sita mbele ya mahakama ya Jaji Kanyi Kimondo, Jumatano amepigwa faini ya Sh30,000 kwa makosa matatu ya kuandaa, kupakia na kuuza pombe haramu.

Lakini kwa makosa mengine matatu ya wizi wa kutumia mabavu, kushambulia akijaribu kuua na ubakaji, John Ngugi Maina amepewa mwaliko tena wa kusikilizwa kwa kesi Mei 5, 2021.

Mshukiwa alijipa umaarufu wa kijambazi kupitia uvamizi wa mauti akiwa na genge la kujihami kwa mishale na mapanga katika mji wa Maragua na viunga vyake ndani ya Kaunti ya Murang’a.

Afisa mchunguzi katika kesi hizo Bw Cleophas Juma-Mangut akiwa ndiye Kamanda wa Kituo cha Polisi cha Maragua alikuwa amewasilisha hati yake ya kiapo mbele ya mahakama akimtaka hakimu asimwachilie mshukiwa “kwa kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yake kwa kuwa raia wanapanga kumuua.”

Aidha, Bw Mangut aliambia mahakama kuwa maafisa wake wana kibarua kigumu kutuliza hasira za baadhi ya wakazi ambao wamepania kuchukua hatua mkononi kumwangamiza mshukiwa pamoja na kuharibu boma lake katika kijiji cha Maica Ma Thi.

“Huyu mshukiwa anafaa apewe hifadhi tu katika rumande akifuatilia kesi kuhusu mashtaka yanayomkabili kwa kuwa ikiwa ataachiliwa, kuna njama ambazo zinanitatiza sana kuzizima zinazolenga kumgeuza kuwa maiti. Ni mshukiwa ambaye amechosha watu kwa kiwango kikuu na tunalaumiwa kwa kuwakataza kumuua. Ni kwa manufaa yetu kama serikali na kwake kama binadamu abakie ndani akifanya kesi zake,” akasema Bw Mangut.

Bw Maina alitajwa kuwa mshukiwa hatari ambaye pia hakuna uhakika kana kwamba angerejea kortini kujibu mashtaka dhidi yake ikiwa angeachiliwa kwa dhamana.

Aidha, alitajwa kuwa hatari sana kwa walalamishi na mashahidi.

Katika kuzingatia masuala hayo, hakimu aliagiza kwamba makosa matatu yanayoambatana na pombe yaorodheshwe kuwa madogo kwa mujibu wa masharti ya Covid-19 na atozwe faini ya Sh10,000 kwa kila kosa badala ya Sh50,000 ambazo ni kigezo katika mahakama nyingi kwa kila kosa la kujihusisha na biashara ya pombe kwa kukiuka sheria.

Hata hivyo, hakimu amesema kuwa makosa hayo mengine ni mazito na yanahitaji umakinifu wa kisheria kwa kuwa “kuna watu walipokonywa haki zao za kimsingi na mshukiwa na ni busara utaratibu kamili wa haki uzingatiwe.”

Katika msingi huo, Maina ameagizwa kufika mbele ya mahakama Mei 5 ili uamuzi wa ikiwa ataachiliwa kwa bodi uafikiwe ili afuatilie kesi akiwa nje au akinyimwa, aendelee kuwajibikia mashtaka hayo akiwa rumande.

Mshukiwa huyo alinaswa Jumamosi baada ya kuhepa mitego ya polisi kwa miaka miwili mfululizo.

Kunaswa kwake kulitokana na yeye kuamua kusherehekea sikukuu ya Pasaka kwa kulewa kupindukia na akaanza safari gizani kuelekea nyumbani kuonana na mkewe.

Katika safari hiyo ya ulevi, alianza kuimba nyimbo za kivita mwendo wa saa nane usiku na hapo ndipo majirani waliokuwa wakitegea kusaidia polisi kumnasa.

Awali maafisa waliahidi yeyote ambaye angesaidia kwa kutoa habari muhimu za kuwawezesha kumkamata mshukiwa angepokea Sh50,000.

Kwa ujumla, polisi walilipa Sh58,000 kwa kuwa wa kwanza kupiga simu alipewa Sh50,000 huku wengine wanne waliopiga baadaye wakipokezwa kitulizo cha Sh2,000 kwa kila mmoja.

Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Bw Anthony Keter ametoa amri kwamba mashahidi na walalamishi walindwe kwa karibu baada ya kuibuka kuwa kuna jamaa, marafiki na wafadhili wa mshukiwa ambao husihi katika miji ya Maragua, Mugumoini na Ichagaki ambao wanalenga kulipiza kisasi.

“Itakuwa ujinga wa hali ya juu kwa yeyote kujaribu kulipiza kisasi. Tuko na ufahamu wa wote ambao wanatoa matusi na kuongea vibaya kuhusu kukamatwa kwa Maina. Hatutasita kuwakamata hata hao na kuwashtaki kwa makosa mbalimbali,” akaonya.

You can share this post!

Ajali ya mabasi mawili Kwa Shume yasababisha vifo vya si...

SAUTI YA MKEREKETWA: Viongozi Afrika hawana punje ya...