Kimataifa

Mwanamume anyongwa na nyoka akimuosha, wazikwa pamoja

July 3rd, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

INDONESIA

MWANAMUME aliripotiwa kufa baada ya kunyongwa na nyoka wake, alipokuwa akijaribu kumuosha.

Mwanamume huyo wa miaka 42 kwa jina Jana alipatikana na mwanawe akiwa maiti, baada ya nyoka huyo kumnyonga kwa kujikunja na kujikaza mwilini mwake, alipotaka kumuosha.

Wanakijiji wenye ghadhabu walifika na kumuua nyoka huyo kufuatia kisa hicho. Mwanamume huyo, hata hivyo, alizikwa pamoja na nyoka wake huyo, ambaye amekuwa akimlea.

Jana anaaminika kuwa alikuwa akimuosha nyoka huyo Ijumaa asubuhi, katika kijiji cha Citiru, wakati kisa hicho kilipotokea.

Akishindwa kuamini ukweli wa mambo, mkewe Jana alisema “Bado najaribu kuamini kuwa mume wangu aliuawa na nyoka.”

Mkewe alisema kuwa alikuwa na hulka ya kuwalea nyoka kisha kuwauza wanapokua.