Afya na Jamii

Mwanamume aomba asaidiwe kufa sababu ya mahangaiko ya kuugua selimundu

February 20th, 2024 2 min read

Na HELLEN SHIKANDA

MWANAMUME anayeugua maradhi ya selimundu sasa amehiari kufa ili apate utulivu kutokana na uchungu anaopitia baada ya kuugua kwa miaka 26.

Joe Mudukiza, ambaye atatimu umri wa miaka 29 hapo Agosti 15 mwaka huu, ameamua kukaidi jamaa na marafiki zake, mila na tamaduni na sheria mbalimbali ili kupata kitulizo katika ulimwengu wa wafu.

Ndiposa ameamua kusafiri hadi Ubelgiji ambako huduma za watu kuuawa kwa hiari hupatikana, chini ya mfumo thabiti wa sheria.

“Tangu nilipopatikana na ugonjwa wa selimundu zaidi ya miongo miwili iliyopita, maisha yangu yamejaa dhiki.

“Japo nimezoea hali hii, uchungu huo umekuwa ukiongezeka kadri umri wangu unavyoongezeka.

“Kwa hivyo, tangu Aprili mwaka jana, maisha yangu yamechukua mkono tofauti, uchungu umezidi,” akasema.

“Nimejaribu njia zote za kupunguza uchungu huo lakini sijafaulu. Nilisaka kwenye intaneti na kupata suluhu- euthanasia, ambayo watu huita kufa kwa hiari (kifo cha huruma).

“Siku moja nilipokuwa nikiishi na binamu zangu Kasarani (Nairobi) nakumbuka nikizingirwa na wauguzi ambao walijaribu kutafuta mishipa yangu ya vena ila walishindwa licha ya kwamba uchungu ulikuwa ukiongezeka kila dakika,” Mudukiza akaambia Taifa Leo kwenye mohajiano ya kipekee.

Alisema amewahi kutizama video na kusoma machapisho kuhusu kifo cha hiari na hivyo basi kupata ufahamu mkubwa kuhusu harakati hiyo.

“Kwa kuwa sheria za Kenya hazitambui njia hii ya kutamatisha uhai, ndiposa niliwasiliana na Chama cha Wanaosaka Haki ya Kufa kwa Hiari nchini Ubelgiji. Wamenipa majibu mazuri na nimeanzisha mchakato huo ila hakuna aliye karibu nami anayeunga mkono hatua hii,” Mudukiza anaeleza.

Anaongeza kuwa madaktari wake wote nchini Kenya, ambao wanapaswa kutia saini mojawapo ya stakabadhi zinazohitajika kabla ya kuuawa Ubelgiji, wamekataa kuhusishwa na mpango huu wa “kumpeleka kaburini”.

“Waliniambia kwamba wako katika taaluma ya kuokoa maisha na sio kuyatamatisha,” Mudukiza akaeleza.

Hata hivyo, alipata hakikisho kutoka kwa madaktari hao wa Ubelgiji kwamba anaweza kutimiziwa tamanio lake bila sahihi kutoka kwa madaktari wake nchini Kenya.

“Kile ninachopaswa kufanya ni kuthibitisha bila tashwishi yoyote kwamba hali yangu ya kiakili ni nzuri na kwamba hatua hiyo ni suluhu yangu ya mwisho,” Mudukiza akaongeza.

Anasema mama yake alipata habari kuhusu uamuzi wake siku tano baada yake kutuma ujumbe kupitia kwa mtandao wa Facebook akielezea nia yake.

“Ujumbe huo ulimshtua mamangu. Alinitumia ujumbe akinikumbusha kuwa yeye ndiye mzazi wangu wa kipekee na akanishauri niende kwake kwa ushauri ikiwa nimezongwa na mawazo,” Mudukiza akaeleza.

Mgonjwa huyu anafichua kuwa ni hadi alipojiunga na shule ya upili ambapo mama yake alimfichulia kuwa amekuwa akiugua ugonjwa wa selimundu.

Hata hivyo, Mudukiza anaongeza kuwa, “Niliendelea kutia fora masomoni na hata nikapita mtihani wangu wa kidato cha nne (KCSE) na kujiunga na Chuo Kikuu, ambako nilisomea shahada ya kwanza ya Kiingereza na Fasihi.”