Mwanamume apata majeraha kwa kugongwa na gari Thika Road

Mwanamume apata majeraha kwa kugongwa na gari Thika Road

Na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mmoja anauguza majeraha baada ya kugongwa na gari mnamo Jumanne wakati akipita eneo lisilo na daraja wala kivuko maalum cha waendao kwa miguu, Thika Road.

Ajali hiyo iliyotokea kati ya mtaa wa Githurai na Roysambu, ilihusisha gari la shirika moja linalotoa huduma za kijamii.

Kulingana na walioshuhudia, jamaa huyo ambaye hawakumfahamu aligongwa akijaribu kuvuka leni ya kasi, Thika Superhighway.

“Niligutushwa na kishindo cha gari dereva akikanyaga breki. Hii si barabara ya kutania,” akasema mchuuzi mmoja wa miwa pembezoni mwa barabara hiyo.

Watu wenye huruma walimpeleka hospitalini ili aanze kupokea matibabu ya dharura.

Kisa hicho si cha kwanza kushuhudiwa Thika Road, wapita njia wakihimizwa kutumia daraja au vivukio maalum vya watu.

“Ukigongewa eneo lisilo na daraja wala alama za pundamilia utalaumu nani? Watu wawajibike na kupitia vivukio vinavyofaa,” akashauri afisa mmoja wa trafiki.

Baadhi ya watu wenye mapuuza wamepoteza maisha na wengine kuachwa na majeraha mabaya kwa kupitia sehemu zisizo na daraja wala alama za vivukio vya barabara Thika Road.

You can share this post!

Wachimbaji mawe Lamu wataka serikali ipige jeki shughuli zao

Visa 40 vya maambukizi ya Covid-19 vyaripotiwa miongoni mwa...