Habari Mseto

Mwanamume apatikana amefariki katika seli Zimmerman

February 27th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

FAMILIA ya mwanamume mmoja inalilia haki ikitaka kuelezwa alivyojitia kitanzi jamaa wao kwenye seli.

Mwanamume huyo aliyetambulika kwa jina Antony alipatikana amejinyonga kwa mshipi jana asubuhi, kwenye seli ya kituo cha polisi cha Zimmerman, Nairobi.

Inasemekana jamaa huyo ambaye ni keateka wa ploti moja eneo la Zimmerman, alitiwa nguvuni Jumatatu usiku kwa kile kinatajwa kama “kuzozana na mke wake”.

Baadhi ya wapangaji waliambia ‘Taifa Leo’ kuwa kabla kukamatwa, mwanamume huyo pamoja na ndugu zake wa kiume na marafiki walishambulia mkewe, wakidaiwa kuwa walevi.

“Walikuwa wamefunga mlango, na tukio hilo lililazimu majirani kuita maafisa wa polisi ili kumuokoa,” akasema mpangaji.

Aidha, inaarifiwa kwamba hata baada ya kukamatwa jamaa alionekana mwenye kiburi na kutishia maafisa wa polisi.

Muktadha aliojitia kitanzi ungali kitendawili, ikizingatiwa kuwa mshukiwa yeyote wa uhalifu anapotiwa seli hushurutishwa kutoa mshipi, kiatu kimoja, na vifaa vyote vya chuma ikiwa ni pamoja na pesa na simu.

“Tunachotaka ni kuelezwa alivyojitia kitanzi baada ya kupelekwa seli,” akasema mmoja wa jamaa zake.

Mbali na jamaa zake wa karibu, hakuna aliyeruhusiwa kuingia katika kituo hicho cha polisi wakiwamo waandishi wa habari.

Visa vya washukiwa kuripotiwa kujitia kitanzi kwenye seli, maafisa wa polisi wakihusishwa kuwadhulumu si vigeni.