Habari Mseto

Mwanamume aponea kifo kwa kudaiwa kuiba pikipiki

April 25th, 2024 1 min read

NA OSBORNE MANYENGO

MWANAMUME mmoja aliponea kifo tundu la sindano baada ya kushikwa akidaiwa kuiba pikipiki ya mhudumu wa bodaboda mjini Kitale mnamo Jumatano.

Kizaazaa kilitokea mwendo wa saa kumi na mbili na dakika kumi jioni katikati mwa mji wa Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia.

“Mwendeshaji pikipiki alikuwa amesimamisha bodaboda yake kwa steji ya Nyayo Market iliyoko mkabala na dukakuu la Khetias Gigamart ambapo mshukiwa alichukua na kuanza mwendo,” akasema mmoja wa walioshuhudia tukio hilo na ambaye hakutaka kutajwa jina.

Mwenye pikipiki kushtuka chombo chake cha kujitafutia riziki hakiko, aliomba msaada kwa wenzake na kuanza kufukuzana na mshukiwa wa wizi.

Walimnyaka mshukiwa akiwa amesonga mwendo wa mita 500 tu.

Alipoona anakaribia kushikwa alisimamisha pikipiki na kutimka mbio kwa miguu, lakini  hakuenda hata mita moja ambapo alishikwa.

Wanabodaboda walimrushia mangumi na mateke lakini kilichomuokoa ni mwenye pikipiki kuwasihi wenzake kumuacha.

“Aliona cha maana ni kuwa alikuwa amepata pikipiki yake na pia mshukiwa alionekana mdogo kiumri na pengine kijana wa kurandaranda mtaani,” akasema shahidi yule aliyeona kilichojiri.

Kisa hiki kilitokea saa chache baada ya askari wa kaunti almaarufu kanjo kujaribu kuwafukuza vijana kadhaa wa kurandaranda mtaani kutoka katikati mwa mji..

Umati mkubwa ulifika kushuhudia kisa hicho.

“Ana bahati hakufanyia kitendo hicho Matisi au Mitume maana huko angekuwa jivu kwa dakika kumi tu,” ikasikika sauti ya mwanamume mmoja kutoka kwa umati.

Mwingine alisema mshukiwa huyo anafaa kuMshukuru Mungu na asijaribu tena kuendelea na maovu hayo.