Kimataifa

Mwanamume ashinda Sh120 milioni mara mbili

June 11th, 2018 1 min read

Na AFP na VALENTINE OBARA

PARIS, UFARANSA

MWANAMUME Mfaransa ameshangaza wengi kwa kushinda dola milioni 1.2 (Sh120 milioni) mara mbili katika kipindi cha miezi 18 mfululizo kwenye mchezo wa bahati nasibu.

Gazeti la Le Paririen lilisema mwanamume huyo ambaye hakutajwa, kutoka eneo la mashariki mwa Haute-Savoie, alipata tikiti za uchindi Novemba 11 2016 na Mei 18 mwaka huu kupitia mchezo wa bahati nasibu wa My Million.

Wataalamu wa michezo hiyo walinukuliwa kusema ni vigumu sana kwa mtu kushinda mara mbili katika kipindi hicho kifupi na haieleweki jinsi mwanamume huyo alibahatika.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza tukio kama hili kushuhudiwa kwani mwezi uliopita mwanamume kutoka Australia alishinda mara mbili katika wiki moja.

Mwanamume huyo aliye na miaka ya arobaini kutoa mtaa wa Bondi alishinda dola 770,000 (Sh77 milioni) kisha akashinda dola 1.5 milioni (Sh150 milioni) katika kipindi cha siku tano.