Habari za Kitaifa

Mwanamume ashtakiwa kumtishia gavana atoboke Sh240m

March 21st, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAMUME ameshtakiwa kwa kudai kwa vitisho Sh240 milioni kutoka kwa Gavana wa Kakamega Fernandes Odinga Barasa.

Kulingana cheti cha mashtaka, William Simiyu Matere almaarufu ‘Elijah’ alimtaka gavana huyo ampe mamilioni hayo ya pesa.

Shtaka halikusema ni vitisho vya aina gani ambavyo Matere alitoa kwa Bw Barasa hata akamtaka atoboke Sh240 milioni.

Mshtakiwa aliyefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Anne Mwangi, alikana mashtaka mawili kwamba alidai apewe pesa hizo kati ya Desemba 2023 and Machi 18, 2024.

Mshtakiwa aliyekamatwa mnamo Machi 19, 2024 na kufikishwa kortini Machi 20, 2024, alikana mashtaka yote mawili.

Mahakama ilifahamishwa kwamba Matere alikula njama ya kumtapeli Bw Barasa pesa hizo akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani.

Matere aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “nitafika kortini siku ya kusikilizwa kwa kesi ama wakati wowote mwingine ule nitakapotakiwa na mahakama”.

Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana ila hakimu aliombwa atilie maanani kiwango cha pesa mshtakiwa alikuwa anadai apewe.

Bi Mwangi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni.

Kesi itatajwa Machi 27, 2024, itengewe siku ya kusikilizwa.