Habari

Mwanamume ataka kumtaliki mkewe aliye jela

August 20th, 2019 1 min read

Na KATE WANDERI na JOSEPH OPENDA

MWANAMUME mmoja amewasilisha kesi katika mahakama moja ya Nakuru akitaka kumtaliki mkewe wa pili anayepatikana na hatia ya kumuua, kinyama, mtoto wa mkewe wa kwanza mwaka 2000.

Bw James Waithaka Muiruri sasa anaitaka mahakama kumpa idhini ya kutalikiana na Hannah Wangari Mungai aliyemuua mvulana huyo mwenye umri wa miaka 16, nyumbani kwao katika shamba la Arash, kaunti ya Nakuru Septemba 18, 2000.

Katika kesi aliowasilisha Machi 18, 2019, Bw Waithaka anaomba talaka kwa sababu ndoa yake haiwezi kudumu kufuatia kitendo hicho cha mkewe wa pili, kilichopelekea mahakama kumpa hukumu ya kifo.

“Hukumu ya kifo iliyotolewa kwa Bi Wangari baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto wa mke wangu wa kwanza, nahisi kuwa ndoa yetu imevunjika kabisa na hamna nafasi ya kuiokoa,” akasema Bw Waithaka kwenye stakabadhi alizowasilisha kortini.

Bi Wangari amekuwa gerezani baada ya kupewa hukumu ya kifo na mahakama moja ya Nakuru mnamo Julai 24, 2004.

Aliolewa na Bw Muiruri mnamo 1993 katika ndoa ya kitamaduni na wakapewa cheti cha ndoa.

Mwili watiwa guniani

Upande wa mashtaka ulisema, mwanamke huyo alimkata kwa panga mvulana huyo na kuweka mwili wake ndani ya gunia.

Baadaye alificha gunia hilo miongoni mwa magunia ya viazi ndani ya stoo jikoni.

Mama wa marehemu, mke wa kwanza wa Bw Waithaka, alitoweka nyumbani mnamo 1995 kufuatia ugomvi wa kinyumbani na kuwaacha watoto wake wanne.

Watoto hao waliachwa chini ya malezi ya mke wa pili, Bi Wangari.

Kulingana na hukumu iliyotolewa na Jaji Alnashir Visram mnamo 2004, ilibainika kuwa Bi Wangari hakuwa akielewana na watoto hao wanne wa mke mwenzake na aliwachukia zaidi.

Alikuwa akiwagombeza kila mara kiasi kwamba aliwafukuza kutoka nyumba kuu ili waishi katika nyumba nyingine katika ploti hiyo.