Habari za Kaunti

Mwanamume atiwa mbaroni mjini Kisii kwa kujifanya wakili

June 8th, 2024 2 min read

NA RUTH MBULA

MWANAMUME mmoja ametiwa mbaroni na polisi mjini Kisii baada kwa kujifanya wakili.

Kwa mujibu wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) – Tawi la Magharibi mwa Nyanza Kusini na polisi, mshukiwa Bw Benard Cheki Matware amekuwa akiendesha kazi ya uwakili kinyume cha sheria kwa jina la ‘Omariba and Company Advocates’.

Bw Cheki alikuwa ameenda kwa afisi ya Msajili wa Ardhi Kaunti ya Kisii, Bw Charles Ayienda, ambaye ndiye aliwapa polisi maelezo yaliyosaidia kumkamata.

“Msajili wa Ardhi, Bw Charles Ayienda aliripoti kwamba mtu aliyemshuku kuwa wakili feki, alienda afisini mwake akisema alikuwa akifuata maagizo ya mteja wake, Venny Bosibori Ezekiel,” Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii Bw Charles Kases alisema Jumamosi.

Mshukiwa huyo alikuwa ameenda afisini kumsaidia mteja ambaye hajui utaratibu wa kupata hati za kuuza ardhi, na kwa mujibu wa polisi, alijipatia Sh40,000 kutoka kwake.

Bw Ayienda alipomuuliza mshukiwa ni lini alianza kufanya kazi ya uwakili, alishindwa kueleza na hata hakutoa cheti cha kazi ya uwakili.

Soma Pia: ‘Wakili feki’ Brian Mwenda kusherehekea Mashujaa Dei katika rumande jijini

Bw Kases alisema mshukiwa alikamatwa katika afisi ya ardhi na kupelekwa katika seli za polisi.

“Fomu ambazo zilitiwa saini na mshukiwa zilipatikana kutoka kwa mshukiwa,” Bw Kases akaarifu.

Mwenyekiti wa LSK wa Tawi la Magharibi mwa Nyanza Kusini, Bw Benard Gichana, Katibu Mkuu Justus Maeche na wakili George Morara, waliongoza wanachama wao kuwaonya watu wanaojifanya kuwa mawakili katika eneo hilo, wakisema watakiona cha mtema kuni.

“Tulipopata fununu kuhusu jambo hilo, tulienda katika afisi ya ardhi ambapo mshukiwa alibadilisha maelezo na kudai kuwa yeye ni karani katika kampuni ya uwakili. Alikuwa na hati kadhaa, ikiwemo mikataba ya uuzaji wa ardhi na fomu za uhamisho wa mali,” Bw Gichana alisema.

Bw Maeche naye alisema tukio la aina hiyo huenda likaondoa imani ambayo wananchi wameweka kwa mawakili katika harakati zao za kutafuta haki.

“Mteja alikuwa amelipa ushuru wa stampu mnamo Machi lakini shughuli yake ilikuwa bado kukamilika,” Bw Maeche akasema, akiongeza kuwa hawataruhusu mtu yeyote ambaye hajahitimu na ambaye hajasajiliwa kufanya kazi kama wakili katika eneo hilo.

Bw Kases alisema mshukiwa atafikishwa kortini kujibu mashtaka ya kujifanya wakili na kujipatia pesa kwa udanganyifu.

[email protected]