Habari za Kitaifa

Mwanamume atupwa rumande kwa kushindwa kulipa bili hotelini

January 12th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAMUME aliyekaa katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi kwa siku 12 akimsubiri mpenzi wake washerehekee sikukuu ya Mwaka Mpya 2024 ameshtakiwa kwa kushindwa kulipa bili ya Sh466,965.

Sasa makao ya Bw Leavan Namayi Lubanga kutoka Kaunti ya Homa Bay yatakuwa ni gereza la Industrial Area alipopelekwa kuzuiliwa akisubiri kesi aliyoshtakiwa isikilizwe na kuamuliwa.

Bw Lubanga alitiwa nguvuni na polisi mnamo Januari 11, 2024, kutoka hoteli ya Pan Pacific iliyoko eneo la Westlands, Nairobi baada ya kushindwa kulipa bili hiyo ya Sh466,965.

“Mheshimiwa nilidanganywa na mwanamke nimsubiri katika hoteli ya Pan Pacific lakini hakutokea. Nilimsubiri kwa siku 12. Nimeshindwa kulipa bili ambayo inajumuisha ada za mlo, malazi na vileo,” Bw Lubanga alimweleza hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe.