Habari za Kaunti

Mwanamume awindwa kwa kudaiwa kuua watoto wake watatu na mjakazi

March 2nd, 2024 1 min read

NA VITALIS KIMUTAI

POLISI Kaunti ya Bomet wanamsaka mwanamume mmoja ambaye inadaiwa aliwaua watoto wake watatu na mfanyakazi.

Mwanamume huyo anadaiwa kutekeleza mauaji ya wanne hao katika kijiji cha Kipkebe eneobunge la Bomet ya Kati, kisa ambacho kimezua taharuki katika eneo hilo.

Inadaiwa mwanamume huyo aliwaua wanne hao Ijumaa usiku kwa kuwakatakata kwa panga.

Mshukiwa huyo alitoweka baada ya kutekeleza unyama huo huku maafisa wa usalama wakisema wana imani kwamba watamkamata.

Kifungua mimba wao alinusurika kwani alijificha nyuma ya pazia wakati baba alitekeleza unyama huo.

Aliwaita majirani alipokuwa akimkimbiza mdogo wake aliyejeruhiwa katika hospitali ya karibu ya Chelymo ambapo alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya Tenwek kwa matibabu maalum.

Mamia ya wanakijiji walimiminika kwenye boma hilo kushuhudia tukio hilo.

Naibu Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bomet, Bashir Ali na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai Geoffrey Omwenga walithibitisha kisa hicho katika kikao na wanahabari kilichofanyika katika kituo cha polisi cha Bomet.

“Polisi walipokea habari kuhusiana na kisa hicho na tumeanza uchunguzi. Tunamsaka mwanamume huyo na tunaamini kuwa atakamatwa,” Bw Bashit alisema.

Polisi waliwataja waathiriwa wa shambulio hilo kuwa – Lewis Kipngeno,14, Lulu Cheruto,2, Abigael Cherono aliyekuwa na umri wa miaka minane na Sharon Chepkoech wa umri wa miaka 16 ambaye alikuwa ni msaidizi wa nyumbani.

Marehemu Lewis Kipngeno,14, aliyeuawa pamoja na Lulu Cheruto,2, Abigael Cherono aliyekuwa na umri wa miaka minane na Sharon Chepkoech wa umri wa miaka 16 ambaye alikuwa msaidizi wa nyumbani. PICHA | VITALIS KIMUTAI

“Wanne hao walikatwakatwa na panga. Tuna imani kwamba tutamkamata mshukiwa licha ya kuwa amejificha,” Bw Bashir alisema.

Mshukiwa huyo anasemekana kwenda katika duka linaloendeshwa na mkewe, Naomi Chepkoech, katika kituo cha biashara cha Silibwet, muda mfupi kabla ya kutekeleza uhalifu huo, na kumsihi afunge duka waende nyumbani.

Hata hivyo, mkewe alikataa.

Miili ya waathiriwa hao imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Longisa ili kuhifadhiwa kabla ya upasuaji wa maiti kufanyika.