Makala

MWANAMUME KAMILI: Acha wakuite zumbukuku ila wasijue yanayokubana kifuani

July 5th, 2019 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

JAMANI debe tupu ndilo litikalo!

Mbona kuingilia ya watu ilhali yetu tumeshindwa kumudu? Mbona kusema ya wengine ilhali yetu tumeficha kwapani? Hebu tusitisheni hivi vita dhidi ya makasisi!

Makasisi pamoja na wahudumu wa maabadani ni wanadamu kama wengine wote.

Katika ubinadamu huo kuna unyonge unaomfika mtu na athari zake. Hivyo basi watumishi hawa hawastahili kejeli na dhihaka kama wanavyofanya kina yakhe wa leo. Nani alisema kwamba kasisi hawezi ghadhabika ama hata kumpa talaka mkewe? Jamani tuzingatie yetu na tuyaache ya watu!

Tumekuwa watu sawa na ngoma! Imekuwa nadra kuona watu wakitulia na shughuli zao pasipo kutangaza ya watu ama kumwaga siri za kwao kwenye kuku wengi mitaani.

Hizi kelele za chura ni ishara ya waja kukosa la tija ama kutafuta kusikizwa japo hakuna la maana litokalo kinywani.

Ni ishara ya wanaume tepetevu, wavivu na domo kaya. Ndivyo walivyo wanaume wa leo. Ikiwa chura anazo akili na hekima kunyamaza sembuse wanadamu watu wa hadhi?

Unyamavu ni hekima tena sifa adimu kwa mwanamume wa leo. Kama hatusemi ya watu, ndio kwanza vifua tunapiga kutangaza sifa zetu. Mwanamume majisifu ni kero! Kina yakhe wa leo wasiojua kufyata vinywa na kudhibiti ndimi zao wanaweza kukupa wazimu. Neema ya ulimi hali kadhalika uwezo wa kuzungumza sio halalisho kwa mwanamume kupayuka na kuboboja ovyo kama wanavyofanya madume siku hizi. Hata ya jikoni anayajulia kuliko mwenye jiko. Kazi gani ya mke ikiwa mume ndiye mjuvi wa yote?

Mwanamume kamili hana budi kukuza akili tulivu na mawazo chanya yatakayomwezesha kufurahia maisha na kuimarisha hadhi ya familia yake. Sharti kukuza na kuendeleza tabia zinazodumisha hadhi ya mume! Mbele ya watu mume hana budi kuwa mnyamavu, mwenye hekima kutathmini hali kabla kutamka neno.

Hizo ndizo sifa za mume mwenye kukufanya mtu mbele ya watu.

Utamtambua mwanamume kamili kutokana na jinsi anavyojizatiti kudhibiti sio tu kinywa na ulimi bali pia hisia na fikira potovu. Wacha watu wakuite zumbukuku lakini wasijue yanayokubana kifuani.

Ndio maana kasuku sio mtu licha ya kuwa mwingi wa maneno!

Katika hadhara mwanamume kamili hana budi kuwa msikivu na mtulivu angalau kutumia muda wake kushika mawili kati ya mengi yanayosemwa na wanenaji.

Tatizo ni kwamba hawa wa leo wamempiku kasuku! Wanajifanya kujua kila kitu na kila neno duniani ila maisha yao binafsi.

Hawa ndugu zetu hawaambiliki hawasemezeki. Hawashauriki katu! Mitaa na nyumba haikaliki kwa kero na ubishani. Sijui kinachowasha ndimi za wanaume wa leo. Jambo lisilowahusu wanaliteka na kujenga mada ya ubishani na ugomvi.

Maisha ya mapadri na makasisi yanamhusu nini mtu ambaye hana mbele wala nyuma? Ndio hawa hawa wanaotangaza talaka za wengine ilhali wenyewe hawajui hata kisogo cha mke.

Na sio kuboboja tu kunakoudhi. Siku zote mwanamume haachi kujishaua. Kitu kidogo cha mume kumezea moyoni, dunia nzima itasikia. Akipanda cheo, mtu hamezi mate.

Akitunga mimba wakunga hawalali kwa taarifa zisizokwisha. Akinunua gari wapita njia walaani kwa tifuo la vumbi. Jamani debe tupu ndilo litikalo! Wanaume, acheni kutika!

Kuna hatari kubwa kuishi na mwanamume kasuku. Rahisi sana kutibua amani kwa ugomvi ama kuchochea chuki mitaani. Hajui maneno ya asubuhi wala jioni.

Maamuzi ya nyumbani hayana maafikiano. Hakuna kujitolea kwa maslahi ya wawili. Hizi ndizo sababu za wengi kuchepuka na kutafuta hifadhi na liwazo kutoka nje ya ndoa! Unyamavu hudumisha ndoa. Likisikika, neno liwe zito linalostahili muda kusilikilizwa. Hizo ndizo akili za mwanamume kamili.

Mwanamume mjuvi haishi shaka. Mwepesi kutunga na kubuni fikira za kitoto. Acheni kubuni ya watu ilhali yenu yanangoja suluhu. Mwanamume kamili hujua hekima ya kinywa kukifyata. Ama ni ile kauli ya nyani kutoona ngokoye!

[email protected]