Makala

MWANAMUME KAMILI: Heri maisha ya upweke kuliko kunichoma moyo

November 7th, 2020 2 min read

Na CHARLES OBENE

KUKOSEWA heshima kwaweza kumkeketa mtu maini sisemi kumpagaza wazimu.

Heshima ndio nguo inayostiri hadhi ya mja. Hata hivyo, hakuna kosa linalostahili adhabu ya kinyama! Mtu ni utu

Visa vya udhalimu ndan i ya nyumba vimekithiri mno. Kama sio mke kupigwa kinyama, ni mwanamume kuchomwa mwili kwa maji ya moto. Kama sio mwanamke kudungwa kisu ni mwanamume kupangiwa njama ya kuuawa. Kulikoni nyie waja mliogeuka hayawani?

Unyama huu umesababishwa na tabia za binadamu kutosamehe na kutosahau makosa ya wenzao. Haistahili wala haistahimiliki mwanamume kugeuza kosa la kibinadamu kama sababu ya kumdhalilisha na kumwadhibu mke au mpenziwe. Na sio adhabu ya fimbo tu inayoudhi, kumkejeli au kumdhihaki mke kwa vijembe vya maneno kwaweza kukuzolea balaa.

Mimi mnyonge heri ninyonge lakini sinipige kwa vijembe vya maneno kila mara. Mja hakosolewi kwa cheche za maneno. Isitoshe, masimango huchochea hasira kiasi kwamba mwenzio atafikiria kulipiza kisasi. Moyo wa mja unaweza kuvumilia lakini sijui kwa muda gani!

Tahadharini nyie wenye ndimi za nyoka. Hakuna mwanamke mnyonge anayeweza kuvumilia milele dhiki na kero za mwanamume asiyedhibiti ulimi. Kunyamaza ni ngao tena njia nzuri kusitisha ugomvi. Lakini kununa kwa miezi kadhaa na kukataa kuzungumza na mke ndani ya nyumba eti kwa sababu mmekosana ni ulimbukeni. Kosa halikosolewi kwa kosa. Ufidhuli kama huu ni ishara kwamba mwanamume hana haja kusuluhisha tofauti ndani ya nyumba. Sivyo anavyofanya mwanamume kamili.

Heri tena wanaonuna na kuvimba! Lakini mwenye kuyacheua na kuyarudiarudia mambo yaliyotendeka na ambayo yamekwisha tatuliwa havumiliki. Heri maisha ya upweke kuliko mtu kunichoma moyo na kunitonesha vidonda tumboni!

Yamfaidi nini mwanamume kumdhihaki mke au mpenziwe kwa kumkumbusha makosa ya awali na kumkwaza kwayo? Haiwezekani kung’ang’ania mapenzi ilhali waona ugumu kumsamehe mtu na kuyasahau ya kale. Kwani mapenzi ni nini?

Penye penzi la kweli hakuna kosa lisilokwisha. Penye vichwa vilivyokomaa, hakuna kosa linaloshinda thamani ya mja. Hata kama ni kweli kwamba mkeo alikwisha mpa mwingine buyu lako la asali; itakufaidi nini wewe mgumu wa moyo kumtajia jina la mume mchovyaji au hata kumkumbusha kisa hicho? Tahadhari usijempa nguvu kukupa kipigo cha moyo!

Mke anaposadiki na kukubali kosa na kutaka radhi kwa unyenyekevu, dhihirisha ukomavu kama mwanamume kamili. Unyenyekevu ni ishara ya upendo wa dhati. Jamani upendwapo pendeka! La sivyo utakumbukia kupenda pasipo penzi! Mwanamume kamili hutumia msamaha kujenga upya uhusiano na kufurahia umoja na tofauti baina yake na mkewe.

Falsafa ni moja. Aliyejitweza mnyanyue! Wewe ni nani usiyetaka kumpa mwenzio nafasi ya kujikosoa? Huwezi kudai kuwa mwanamume bora na ubora wako hauna maana wala manufaa ikiwa huwezi kudhihirisha upendo na kumnyanyua aliye chini. Hivyo ndivyo anavyofanya mwanamume kamili.

[email protected]