Makala

MWANAMUME KAMILI: Heri udondoke jasho ukulini kuliko mate madanguroni!

May 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES OBENE

MARA kwa mara tunakumbana na magogo ya wanaume wanaokesha madanguroni na kwenye vilabu vya walevi wanywaji ngongo kama njia ya “kujiliwaza na kupunguza matatizo!”

Baadhi ya walevi wanaolala vilabuni hufanya hivyo ili “kukwepa dhiki na bughudha nyumbani na chumbani.”

Niwieni radhi kuwacheka nyie mahambe wenye “matatizo na dhiki” ambao mnaona heri kufia kwenye mabaa badala ya kufia maabadani! Sijawaona watu zumbukuku zaidi ya wanaume wanaolewa chakari ili “kujiondolea dhiki!”

Hebu tafakari kwa kina akili za baadhi ya wanaume wa leo. Mtu hana hanani si chunguni si mfukoni.

Hajalipa kodi ya nyumba sisemi karo kwa wanawe ambao wamekwisha fukuzwa shuleni.

Mke hana masurufu wala kopo la uji kwa wanawe.

Vipi mtu kama huyu hupata ujasiri kwenda kwenye baa kulewa chakari ama madanguroni “kutuliza akili?”

Jamani nielezeni nyie gwiji wa mambo haya. Nifahamisheni ukweli wa mambo kwamba mwanamume anaweza kupata tulizo kwenye baa ama pajani kupapurana na mashangingi ambao wenyewe wako kazini kuchuma kutoka mifuko ya malofa gumegume wa leo.

Heri mtu kukosa mwili kuliko kukosa akili.

Mara ngapi tumewaona waliolala mitaroni baada ya mbwembwe za unywaji kuwalemaza viungo?

Kuna idadi kubwa ya wanaume wa leo wanaouguza majeraha na makovu ya ulevi ama waliogongwa wakitapatapa barabarani usiku wa manane.

Iweje watu waliotumainiwa kama viongozi nyumbani kuasi majukumu ya uongozi na kuchagua unywaji ngongo kama njia ya kukwepa majukumu? Sasa tafakari dhiki za mume aliyevunjika fupaja ama aliyegongwa barabarani akiwa mlevi chakari.

Ole nyinyi mnaotafuta suluhu kwenye mabaa!

Mwanamume kamili ni mwingi wa utu na ubinadamu. Ubinadamu ni kudumisha mshikamano kujitahidi kiume kujiepusha na hawaa za nafsi.

Hiyo ndiyo tajriba ya mwanamume kamili.

Kinyume na matarajio ya wangwana; tunaishi miongoni mwa wanaume walioasi uongozi nyumbani wakachagua kupapurana na kulumbana kila uchao kama fisi wanaong’ang’ania mzoga!

Mnazozania nini wakati watoto wanalalia mate? Kuna wanawake wanaotafuta wanaume ama wanaume wanaotafuta wanawake lakini wakaambulia mazimwi ya watu!

Mwanamume wa leo mwingi wa usununu na dhiki moyoni. Hafukuliki wala hafunguki roho kinyaa kikamwondokea.

Isitoshe, mwanamume wa leo anaona heri ugomvi kuliko kwenda viwandani kufanya la kijungumeko hata kama ni ukuli ama utopasi!

Heri mwanamume kudondokea kijasho ukulini kuliko kudondokea mate mandanguroni.

Fanyeni la busara nyie gumegume mnaodunisha hadhi ya mwanamume kamili.

Mwanamume wa leo amekuwa hamira kuche kusiche. Anavimba akiiva japo haliki hapakuliki. Nyumbani hasemi hasemezeki. Akiitishwa hatoi, akiulizwa haungami.

Yuko waya

Hana pesa hana posho.

Kuishi na mwanamume asiyejieleza waziwazi ni sawa na kula kitoweo kilichotonewa sumu.

Hivyo ndivyo alivyo mwanamume asiyejua kunena na kujiondolea fundo moyoni. Anaweza kukutia wazimu kabla ya msimu wa kichaa. Tahadharini nyie mnaopenda kupendwa na wanaume mahambe walevi wa leo!

Tatizo kubwa linalosibu maisha ya wanadamu wa leo ni uhasama na uadui unaotokana na udhanifu na uchufu wa mwanamume.

Hivi tulivyodhikika maishani, nani mwenye moyo wa jiwe asiyetaka mpenzi mwingi wa ucheshi, umbuji, unyofu na ucha Mungu? Lakini tuwapate wapi wangwana walioradhi kutukoga sisi tunaopenda maisha fufutende?

Upenyenye na upeketevu wa wanaume wa leo umekuwa ufa unaoporomosha misingi thabiti wa uchumba na uchu wa mahaba.

Hawajui mzaha au ucheshi hawa wanaume wanunaji! Dunia yenyewe ni mwamba wa jiwe.

Mke yupi anayetaka kuishi na jiwe lingine nyumbani?

Na sio unyamavu wa wanaume tu unaochusha maisha ya vimwana wa leo.

Wako gumegume wanaopeleka matatizo ya nyumbani au chumbani na kuyaweka mikekani, akina yakhe kuyajadili na kuyatafuna katika mahakama ya malofa wasiojua kitu ila kumwiga mbuzi kuchana majani ama kumwiga nguruwe kulala mitaroni.

Muda mnaotumia kula raha kwenye mabaa na kwenye madanguro unatosha kuchuma angalau kopo la uji na kuwafaa jamaa na jamii.

Wajibikeni kama mwanamume kamili hasa nyie gumegume walevi wa leo mnaotafuta liwazo na hifadhi kwenye mabaa.

Mwanamume kamili ni mwingi wa utu na ubinadamu.