Makala

MWANAMUME KAMILI: Ilmuradi una uwezo wa kula vya kuliwa, kula shibe yako!

August 3rd, 2019 3 min read

Na DKT CHARLES OBENE

TUMEZOEA mno kuzozana mazishini ama kupigania wali wa ndevu!

Jamani walaji, mbona kutwa kucha mlishindwa kuzoa vya kuzoleka mkafaidi uhuru wenu? Hebu jifunzeni kutoka tabia ya walaji wanasiasa! Wameamua kula mchana wa jua; tupende tusipende!

Sijui mbona hizi tetesi nyingi kwamba nchi inaporwa na walaji wanasiasa hasa! Sisi wananchi tena wenye nchi ndio kwanza tumewapa idhini walaji kuvunja mgongo wa punda. Sisi ndio tumewaridhia kufanya wanavyotaka na rasilimali zetu. Iweje tunalilia vikaoni na kusoneka kama kwamba hatujui walaji? Mwizi kumridhia kukuibia kidogo chako lawama kwa nani? Wananchi waliozembea, tena watepetevu dawa yao hiyo hiyo. Uzembe huleta kilio.

Vivyo hivyo, nawapongeza vichuna waliozindukia majongoo na kuvamia mali na rasilimali ya wanaume wazembe. Dawa ya mume asiyejua kutunza vyake ni hiyo hiyo.

Ilmuradi una uwezo wa kula vya kuliwa, mwanamtu kula shibe yako! Mwanamume aliyeradhi kuliwa sharti kuporomoshwa na kufilisishwa kabisa.

Tujifunze kutoka shughuli za wanasiasa. Tumbo kwanza, fikira na akili baadaye.

Nasema hivi kwa sababu mwanamume wa leo habembelezeki kwa mawele ama mpunga!

Waweza kujitolea mhanga kumhonga mwanamume kwa shehena la penzi, tena yaliyonogeshwa kitanga kama wanavyosema wajuvi wa mapenzi lakini mwishowe utaishia jalalani tena mwingi wa majuto.

Ule usile vya mume wa leo mwishowe utajikuta pembeni huna chako huna wako! Laiti ungalijua mapema labda ungalishibisha nafsi na tumbo kabla siku ya chozi.

Imekuwa jambo la kawaida kushuhudia vituko na vita mazishini baina ya jamaa, jamii, familia au hata baina ya wanawake – kila mtu akijitahidi kutambuliwa rasmi kama jamaa halali wa mwendazake. Mbona kusubiri kifo cha mume kabla kuanza kuzozania mali?

Jifunzeni kutoka tabia ya wanasiasa wa leo. Nchi huliwa ingali nchi!

Vilevile, mwanamume huliwa angali mtu wa pumzi! Wanataka kuliwa baba na babu zenu. Mbona kuwahurumia? Huwa wapi hawa wanawake ambao ndio kwanza wanapigania jukwaani kusikika mazishini? Wanapigania nini hasa ilhali walikuwa na muda wote kufaidi jamaa zao wakati mwanamume alikuwa hai?

Wengine tumetunga usaha kuwakebehi wanawake kufuata mikwanja wasiotolea jasho. Sijui hilo la kutoleana jasho.

Nijuavyo hasa ni kwamba paja lina gharama. Sharti lilipiwe kulikuza, kulikolezea mvuto, kulichezesha au hata kuligusagusa tu. Ndivyo wanavyosema wanasiasa vilevile. Wanatuibia kwa kuwa wanatuhudumia!

Wapo vilevile akina sisi tunaowasuta wanaume wasiotosheka na mke mmoja. Wenyewe walikwisha sema kwamba hawajamwona mja kala mara moja, tena chakula kimoja kikamshibisha kwa mwaka mmoja!

Wanadai ni haki yao kula na kusaza. Hekima ya wajinga haitolewi shuruti! Wacheni wenye haja kula, wale shibe yao. Nao wacheni vichuna wachune shibe yao. Wajapo zinduka, hazina itakuwa pango jinsi taifa hili lilivyosalia sega tu! Hongera nyie walaji!

Miaka ya nyuma, akina sisi – yaani mimi na nyinyi limbukeni wa mapenzi tuliteta kwa hamaki kwamba wanawake wa leo walikwisha janjaruka na wapo duniani kuchezesha kina yakhe mchezo wa pata potea tena potelea mbali.

Hivyo ndivyo tulivyodhani! Ama kweli asiyenakili ya dunia hana akili! Nani bingwa zaidi ya mwanamume wa leo?

Hebu tuyaweke mambo wazi. Dhana kwamba wapo wanaume wakarimu tena walioradhi kumwaga pesa kwa masilahi ya mtoto wa mtu zimepitwa na wakati! Ndio maana wanawake wanasubiri hadi kifo angalau kutafuta haki!

Sina haja kudunisha uwezo na ujanja wa wanawake katika dunia hii iliyojaa pwagu na pwaguzi. Ila nitaweka wazi kwamba ngao ya mke ni kipochi chake! Kijaze kipochi mwanamtu lakini kamwe usiweke maanani kutegemea kitita cha mwanamume wa leo.

Lakini tahadharini nyie mnaokula vya wanaume wa leo. Hakuna mwanamume katika dunia nzima anayeweza kumpa mke vya bure bila kumpangia mikakati jinsi mlaji atakavyolipia lije jua ije mvua. Nyie pwagu hamna chenu mbele ya pwaguzi waliokwisha jua mbinu zote kupata haki zao!

Mara ngapi wanawake wameachiwa magonjwa ya zinaa kama zawadi tosha ya kufuata mafungu ya wengine?

Wangapi wamechomwa visu au kutokomezwa kuzimuni kwa kudai malipo ya paja? Mwanamume wa leo ndiye gwiji katika huu mchezo wa mlaji huliwa! Heri mwanamke kushika yake mpini na mgongo kuupinda shambani kuliko mwenyewe kuwa shamba linalolimwa kama kwamba limejaa magugu!

Kama lazima kula, hamna budi kula vya mume angali mtu wa pumzi! Hata nchi inaliwa ingali nchi! Mwanamume ni mwanamume hadi kifo chake. Tahadharini nyie walaji mnaopigania vya dezo.

 

[email protected]