MWANAMUME KAMILI: Kama lazima kumla mtu jamani msile muda wake

MWANAMUME KAMILI: Kama lazima kumla mtu jamani msile muda wake

 

Na DKT CHARLES OBENE

MZEE mmoja alishangaza wanakijiji mtaani kwetu alipofika kumtwaa mwanawe.

Binti alikuwa keshasema ameolewa ila janadume halijaonekana wala kujiwasilisha kwa wakwe zake. Kuna nini hawa vijana wa leo!

Alipoulizwa mbona hajafika nyumbani hakusita. Alipasua mbarika kwamba hajaamua kumwoa mwanadada! Walafi si haba katika dunia hii isiyokwisha visa na visanga. Kama lazima kumla mtu jamani msile muda wake. Kuna wanaume kwa wanawake wanaojituliza vifuani kwa wengine ilhali wanajua tosha kwamba hawana dhamira wala lengo kudumisha uhusiano ule. Yaani wanaishi kuwahadaa wenzao ilhali ndani kwa ndani wanajua kwamba hawataki kuoa ama kuolewa.

Kila wikendi, wako vibarazani sisemi mikahawani kula vibanzi na kunywa mvinyo. Usiku wa manane, wako chumbani wakiimba nyimbo za mapenzi utadhani wameshikana kama mtu na wake. Hebu niwajuze mbivu na mbichi ya mwanamume kamili. Amekwisha kunipapasa moyo mama, nami nikasitisha ujahili na masomo ya ujanani. Sasa nasubiri ridhaa yake wazazi tukawape tabasamu, pamoja kuwashukuru kwa malezi mema. Mwanamke mwema sio kitabu eti unamsoma.

Hebu tafakari mambo ya leo. Totoshoo anaegeshwa kwenye uchumba akihesabu miaka, miezi, wiki na siku ilhali janadume hajaacha kumtambalia, sisemi kumtembeza kwenye anga za mazimwi. Janadume hachelei kumlambatia kama kwamba ni pipi. Wanapoulizwa mipango ya ndoa, mahambe hawa wepesi kudakia kwamba wangali “masomoni!”

Sitisheni nyie wafidhuli mnaopenda kuwapotezea wenzenu muda kwa manufaa yenu binafsi. Lau tungalithamini mno miaka, miezi, wiki na siku wanazoishi wenzetu, tungaliwajibika na kuwafaa barabara. Tungalisitisha ubinafsi na kuekeza katika maisha yao. Tungalifanya kila jitihada kuboresha maisha ya wanawake na wanaume walioekeza muda wao katika maisha yetu.

Je, wewe ni miongoni mwa binadamu katili wasiothamini muda sisemi kuheshimu miaka, miezi, wiki na siku za mwezi? Nataka kuwaeleza kimasomaso nyie wenye tabia hizi chukizi. Muda aliojaaliwa binadamu una thamani sawa na maisha yake. Ni wajibu wetu kuheshimu muda sawa na mtu mwenyewe. Hivyo ndivyo anavyofanya mwanamume kamili.

Unaweza kumnyoa mtu nywele na kumwachia fuvu pekee lakini baada ya muda mfupi, atakuwa ameota shungi nyingine. Unaweza kumwibia ama kumfilisi mja kitita cha pesa lakini kwa ukakamavu na bidii, anaweza kujijenga imara akatajirika maradufu. Lakini miaka, miezi, wiki na siku alizopoteza mtu hazirudi tena. Kama lazima kumla mtu jamani usile muda wake. Ndio wazo la leo. Kuna wanawake kwa wanaume walioekeza muda wao kutumainia maisha mema lakini mwishowe wakaachwa wamekumbatia viwiliwili. Heri kutapeliwa pesa kuliko kutepeliwa hisia na kusalitiwa.

Nilivyosema awali kwamba mwanaume kumweka maktabani na “kumsoma mke” kwa miaka na mikaka ni ukatili usiomithilika. Vilevile mwanamke kumwegesha mume kama gari kweche pasipo kumpa ridhaa ni ukatili.

Tangu lini binadamu akawa somo ama mabuku yanayosomwa? Tatizo langu ni ujuvi wa hawa “wasomi” wasiojua hata maana ya maisha yao wenyewe. Wanajifanya weledi wa mapenzi wenzao kuwapotezea muda bure. Walisomea wakaelimika wapi ndipo wajifanye weledi wa mapenzi? Walitumia mitaala ipi kuijenga hiyo falsafa duni? Ama ni ule ule uzumbukuku wa kawaida waja kuwapotezea muda bure kabla kuwaegesha mfano wa gari kweche? Msijesahau kwamba mhini na mhiniwa njia yao moja.

Mwanamke umekwisha kumjua nje na ndani lakini bado unahadaa kwamba “unamsoma!” Mwanamume amekwisha kukupa vyote vya kupewa mwanamtu, amekwisha kukutambulisha kwa wote katika jamii na jamaa yake, lakini bado unamhadaa kwamba “unamsoma!” Mbona wanadamu wa leo kujitia ujuvi wa mambo wasiojua mwanzo wala mwisho? Bindamu huwezi kumsoma wala kumjua hadi mwisho wa tabia zake. Haya masomo yasokwisha ni ya nini?

Hizi tabia za wanaume wa mijini na vijijini zinadhalilisha wanawake pamoja na kuwapa jina mbaya katika jamii. Mwisho wa “masomo” haya ya mahambe ni dhiki na sononeko tu. Ndio maana wanawake wengi wamekata tamaa ya ndoa wakaamua wenyewe kubeba ndovu na mkongawe! Walivyodhaniwa kuwa wanaume wenye staha sivyo walivyo hawa gumegume wa mijini. Afadhali tuwaite walivyo.

Matapeli wa mapenzi wanaopenda tu kulishwa halua ila hawana haja kuoa! Kwa hizi tabia za kutia mikono chunguni mboga haijachemka, wanawake wako hatarini kuhimilika hata kabla kujua iwapo wamekwisha fuzu “mtihani wa mume!”

Ole nyinyi ambao mpo uwanjani kutafuta wapenzi na wachumba! Tahadharini maana hawa wetu hawana haja kuoa ama kuolewa! Wako maktabani wenzao kuwasoma tu.

obene.amuku@gmail.com

You can share this post!

UMBEA: Siku hizi makahaba hawapo tena barabarani, wapo...

FUNGUKA: ‘Nacheza mechi za majuu pekee’