MWANAMUME KAMILI: Kila nyumba huwaka moto, muhimu kujenga muamana heshima

MWANAMUME KAMILI: Kila nyumba huwaka moto, muhimu kujenga muamana heshima

NA DKT CHARLES OBENE

Je, ulijua kwamba kutaka kuishi “kama wanavyoishi majirani” ni “uchochezi” unaoweza kuzua rabsha wanandoa wakachaniana nguo sisemi kuvuana heshima hadharani?

Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa katika “nyumba” ya jirani mmoja baada ya vita vikali kuzuka kufuatia “ushauri” wa mke kwa mumewe.

Kwa hakika, sijawahi kusikia wala kuona watu wazima – tena waliokwisha vua soni wakakoga pamoja – wakipigania jambo la kitoto kama lile. Mwanamume mmoja hakusita “kukomesha uchochezi” wa mkewe. Hebu nielezeni nyie mnaojua maana ya “uchochezi!” Alichocha akachochea nini hasa?

Gumegume yule hakuweza kujizuia kiume baada ya “mkewe kumwambia hadharani kwamba ndoa za majirani zilikuwa bora kuliko yao!”

“Majirani walipatana, walipanga mikakati, walifanikisha miradi na kufurahia ufanisi kama familia inavyostahili kufanya!” Isitoshe, mwanamke yule alipendekeza “mumewe kutenga muda na kuwapeleka kujivinjari wikendi” kama “walivyofanya majirani” na “marafiki wa karibu.”

Sijui kama kweli ushauri huu aliotoa “mke kwa mumewe” ulikuwa mbaya ama “ulichochea” kitu. Nijuavyo ni kwamba ndoa za machizi wa leo si ndoa za kujadiliwa kwenye safu ya watu wazima wanaojua maana ya “wawili kuja pamoja na kuwa mwili moja!”

Ndio kwanza tunavuna matunda ya watu kuoa na kuolewa wiki moja baada ya kukutana kwenye dansi za usiku! Hakuna siku mwanga utaoa ama kuolewa na kiza cha maki. Mwanamume kamili anajua tosha vipi na wapi kutuliza mvuke kichwani mwake

Nasisitiza kwamba lililowasha moto wa hamaki watu wazima wakafarakana hadharani lilikuwa jambo la kitoto lisilostahili kuzungumziwa mbele ya watu wazima wenye akili razini.

Lakini kwa kuwa limetishia kuwa chanzo cha vita vya kila siku kwenye nyumba za majahili na machizi wa leo, hatuna budi kulizungumzia na kulikomesha kabla wajuvi wa mitandaoni na kina yakhe kulitilia pilipili. Wajua tena kazi ya wambea wanaopenda mno “kueneza habari” ama kutoa “elimu nasaha” mitandaoni!

Kila nyumba ina siri na kila chumba kimeficha changamoto zake. La muhimu zaidi katika kukuza muamana nyumbani ni kuwepo usuhuba wa dhati na heshima baina ya “mume na mkewe.” Hilo lina maana kwamba wanaooana na kuolewa sharti wazingatie usuhuba kabla ya mapenzi kama kigezo kuu.

Ni jambo la busara mno mwanamume kumchumbia na kuoa rafiki. Vivyo hivyo, mwanamke anastahili kufia rafiki. Mtu unayemjua tena anayekujua nje na ndani katu hawezi kuhamakika ovyo sisemi kutoa ushauri wa kipumbavu katika ndoa. Kuna mambo na tofauti za nyumbani zinazoweza kutatuliwa kwa njia ya “kucheka na kuchekeshana tu!”

Ndivyo maisha yalivyo. Hivyo ndivyo wanavyoishi watu waliotanguliza usuhuba kabla ya mapenzi. Ole nyinyi mliochagua wanawake kwa misingi ya ukubwa wa nyonga! Ole nyinyi mliokimbilia kuolewa na “mastaa tajika katika jamii!”

Usuhuba huu ndio gundi inayoleta watu wazima pamoja wakaona vyema kuweka wazi maisha na siri zao. Usuhuba hauna husuda wala chuki.

Tatizo linalotusibu akina sisi tunaofyatuka kama pomboo ni tabia ya kuoa mashangingi wa vilabuni ama kuolewa na gumegume tunaogutukia kwenye vilabu vya walevi chakari. Kweli, kuoa na kuolewa na mtu usiyejua asili wala fasili yake kama wanavyofanya kina yakhe wa leo ni mwiba unaozidi otesha tende miguuni mwa wanandoa wa leo.

Hakuna na haitakuwepo nyumba ya wawili ambamo hamna zogo japo kidogo. Kutopatana kwa jambo ama wazo miongoni mwa wanandoa ni ubinadamu wala hakuna haja kumaliza kuni kupika na kupakua tofauti hizo mbele ya umma.

Wenzangu watu wazima, msidanganyike kwa hadaa za nyuso za wanandoa zinazometa kama mwezi mkadhani “kwao ndiko peponi!”

Msimalize mate kubishana bure mkitaka kuishi kama “majirani wasiogombana.” Nyinyi mnaoshauriana kupitia arafa za simu ama nyaraka za mitandaoni ndio kwanza “aibu iliyotusibu!” Wanandoa wanaopigania maisha ya majirani wanadunisha mno maana ya ndoa. Hakuna nyumba bora kuliko ya mwingine.

Tofauti ni kwamba “kusikofuka moshi” ni nyumba ya wawili waliokwisha chagua kutumia ubongo kuliko midomo na ulimi. “Majirani wasiogombana” wamechagua wenyewe kujiheshimu na kuzipa hadhi familia zao.

Wamechagua kujenga kuta kuzuia wambea kuchochea maisha ya kwao. Isitoshe, wameekeza kukuza usuhuba na heshima baina yao. Hiyo ndivyo wanavyofanya mwanamke na mwanamume kamili.

obene.amuku@gmail.com

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Kenya, Afrika zitafaidikaje kwa utawala wa...

UMBEA: Mwanamke huridhishwa zaidi na ukarimu na upendo wa...