Makala

MWANAMUME KAMILI: Mahaba bila pato ni kama hadithi ya paukwa pakawa!

August 24th, 2019 3 min read

Na DKT CHARLES OBENE

MWANAMUME kufurushwa nyumbani ndio dawa mujarabu ya wazembe wa leo!

Vituko na visa vya wanaume kutemwa ama kufurushwa kutoka nyumbani vinazidi kuwapa wengi tumbo joto.

“Kuachwa mataani” kama wanavyosema wenyewe, inaelekea kuwa jambo la kawaida hasa kwenu msiojua maana ya mume kushika jembe na mpini wake! Mume wa mwanasiasa kutoka eneo la Pwani ndiye mhasiriwa wa hivi karibuni.

Mwanasiasa yule nusra kumtibua mumewe roho alipomweleza waziwazi kwamba hana lake hana chake. Kisa na maana? Amekuwa “mume wa kawaida asiyetosha mboga!”

Isitoshe, dume lile lilipata mwaliko kwamba “asione hofu kwenda kwa wakwe zake kurudishiwa posa na pesa nyinginezo alizotoa kwa faida ya wazazi” wa mwanasisiasa yule. Hebu niwakumbushe nyie ngiri wenye akili zisizopata kwamba mara ya mwisho mwanamume kulishwa tunda na mke, wote “walifurushwa kutoka shamba lazizi la Edeni!”

Weledi wa mambo wanasema kwamba safari bila changamoto huibua uzembe na udhaifu.

Labda ndio maana baadhi ya wanaume wa leo si wanaume hasa! Kuna aina fulani ya malezi hasa kwa vijanadume wa leo yanayonizidisha hamaki moyoni! Mwanamume kudekezwa na kutendewa kila jambo ndio mwanzo wa dhiki katika familia zijazo! Watajua lini kujituma kiume kama wanafanyiwa kila jambo?

Tumewaacha vijanadume wakilala na kuamkia simu kana kwamba ni kazi ya mume. Isitoshe, wazembe hawa wanafika sebuleni kula tu hata meza kuandaa hawajui kitu.

Hamna chenu nyie wazembe maana vimwana ndio kwanza wanasoma usiku na mchana angalau kujiweka tayari kuutwaa uongozi wa familia. Ukweli ni kwamba mke wa leo mwingi wa hamasa kuliko mume.

Baadhi ya vijanajike wanachukua hatua kujiweka pema siku za usoni ilhali wenzao wa kiume wanashinda mitandaoni wakizuzukia maumbo ya kike!

Hebu niwaonye wanaume wanaolaza damu mikekani huku wamefundika majani ya miraa mashavuni kwamba chuma chao ki motoni!

Watakuja tambua ukweli kwamba mume si mume bila uwezo wa mwanamume kamili. Uzembe haujakuwa wala hautakuwa sifa ya mume.

Ole nyinyi mnaozubaa kucha kutwa na rununu viganjani mkitazama picha za warembo mitandaoni badala ya kwenda kusaka ajira na ujira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Sielewi wala sitaki kuelewa jinsi mwanamume mwenye akili timamu anavyoweza kuzembea ilhali vimwana wanatiririsha kijasho sokoni ama viwandani wakitafuta angalau sarafu za kujikimu.

Kuna familia nyingi zinazotapatapa kushikilia kamba pembamba kutokana hasa na uzembe wa mwanamume ambaye ndiye kichwa na shingo ya familia.

Mwanamume kutowajibikia masilahi ya familia ndio mwanzo wa maisha mawe! Mzigo hauchukuliki wala chumba kuingilika pasipo uwezo wa mume kukidhi mahitaji ya familia.

Hilo nimewapa bure bilashi! Mtakuja kujua kwamba mahaba bila pato ni kama hadithi ya paukwa pakawa!

Kila ninaposikiliza tetesi na kesi za wanaume waliotemwa ama kufurushwa kwa kosa la kutowajibikia familia ama watoto, ninacheka! Msinione mtovu wa nidhamu. La hasha! Mume mzembe hana chake hana lake! Dunia ya leo imejaa gumegume wanaodunisha hadhi ya mume kwa kutopenda kufanya lolote la tija. Uzembe huo ndio mwanzo wa maafa kwa vizazi vijavyo! Mwanamume mwenye pesa ndiye mwanamume mla raha! Nyie wengine ni sawa na kombamwiko mnaobahatisha maisha kuguguna na kutafuna ukavu wa mwiko!

Kwa mwanamume mwenye mali na uwezo wa kukidhia familia huenda heshima na mahaba kochokocho. Ole nyinyi walalahoi mnaofukuzana na watoto wa watu waliosoma wakahitimu vyuoni. Yenu mahaba ni kama mwavuli wa kuazima! Mwisho wa siku atakuja mwenyewe kuutwa na kukuachia zigo la moyo hata mguu kuunyanyua usiweze!

Zindukeni nyie mnaotarajia wanawake kula na kushiba mate ama nyama ya ulimi! Mwanamke akijua yake thamani hana muda kupoteza kumchumbia mwanamume asiyewajibikia maisha yake binafsi na ya familia yake.

Na hilo liwe onyo kwenu mnaopenda wenye ngazi za juu ilhali gumegume huna hunani! Wajibikeni msijekuwa kielelezo cha maisha ya malofa.

Haileti shangwe kuambiwa makuu jinsi mwenzenu mume wa mbunge fulani alivyodhihakiwa “kwenda kutwaa posa!”

Tatizo langu ni kwamba, wanaume wamekuwa vichwa pumba, tena wafujaji wanaokesha kwenye vilabu vya walevi wakinywa na kula mshahara wote kufurahisha vichuna wanaochuna kutoka mifuko yao.

Isitoshe, wanaume wa leo wako mbioni kutafuta na kuwafurahisha wao hao wanaoponda raha na kuwafilisisha wakijua fika kwamba mume mwani hana chake. Hakuna mume wa leo aliye radhi kuekeza jasho lake kwa manufaa ya kesho!

Zindukeni nyie mnaofuja jasho kabla hamjaambiwa kwenda kutwaa vichele vya posa! Mke wa karne hii hana huruma wala mapenzi kwa yeyote asiyetosha mboga! Mwanamume kamili ndiye mboga! Katu hapaliki tonge la sima bila yeye! Mwanamume mwani hana chake!

[email protected]