Makala

MWANAMUME KAMILI: Masuala ya huba, kasoro za maumbile ni siri za moyoni

July 12th, 2019 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

TOFAUTI baina ya wanadamu haziepukiki maishani.

Lakini tutahadhari kumwaga mtama kwenye kuku wengi hasa katika enzi hizi za teknohama!

Isitoshe, sharti watu kukomaa na kuwa wangwana wanaotafuta suluhu pasipo kufedheheshana kwenye mitandao ya kijamii.

Ninasisitiza kwamba kuzungumza kwa uwazi ndio dawa mujarabu inayofungua roho za waja waliodhikika na kujawa hamaki. Napenda sana kuwaona wanaume labizi wakikutana na wazee wenzao kuzungumzia hali ya mambo duniani.

Penye wazee hapaharibiki neno! Isitoshe, kisu hupata makali kwa kushirikiana na kinoo.

Napenda vilevile kusilikiza mazungumzo baina ya wanaume wepesi wa akili; wenye nasaha, hekima na taadhima. Napenda kubadilishana mawazo na watu; wadogo kwa wakubwa wenye ujuzi wa miaka na mikaka angalau nami nijfunze kutoka hekima na mbinu zao.

Siwezi kuwa mwanamume jalili pasipo hekima ya hao walionitangulia duniani. Wala sitaki kuyarudia makosa yaliyoangamiza walionitangulia! Hiyo ndiyo hekima anayostahili kukuza mwanamume kamili.

Tatizo kubwa linalokera ni kwamba wapo wanaume wa leo wasiothamini siri za wenzao. Raha yao kujidunisha mbele ya watu kwa tabia za kutia doa maisha ya wenzao. Midomo kufunguka tu, mwanamume hana haya kutia chuku na kudunisha wenzake.

Kazi yao hasa kukosoa na kudhihaki hadharani wapenzi au hata wanawake ambao kila siku huwavulia sisemi kuwalilia na kuwavumilia kimaisha.

Lini tukawa na mwanamume kasuku? Hana nafasi miongoni mwa waja wangwana wanaotegemewa katika jamii.

Nazungumzia wanaume wanaochukua kosa la mke na kulifanya mada ya mazungumzo katika vikao vya kina yakhe. Ghafla utawasikia wakibweka mambo ya kitoto! “Mke wangu mwingi wa shombo, hunichefua!”….. “Mke wangu gogo! Hajui nianzapo wala nimalizapo shughuli za mume!”…..“Mke wangu limbukeni wa chumbani, hajui kitu!”….. “Mke wangu, mke wangu! Jamani, mkeo atakuaje mada vijiweni?

Semi hizi zinasononesha na kuchefua moyo wa mke. Hakuna mtu mwenye hadhi anayeweza kuvumilia kusemwa na midomo ya waja wasomlisha wasomvisha! Nawasihi nyie wenye kupayuka angalau kusaza mada ya mijadala vijiweni. Ya kwenu hamna budi kuyaacha kwenu! Hiyo ndio hekima ya mawanaume kamili.

Kuna wanaume wenye midomo ya kinanda! Hata kama wewe na mkeo hulala vyumba tofauti, situlishe ya kwenu. Hayo ni mambo ya chumbani ambayo kamwe hayawezi kujadiliwa hadharani. Mkeo awe gogo lisilohisi wala kusisimkia kitu sisemi gwiji mwingi wa mbinu; hayo yote hayatuhusu kitu!

Tatizo kubwa kwa wanaume wa leo ni ulimi mwepesi kunena lakini ubongo mzito kutafakari.

Mambo ya ndoa si mzaha wa kitoto kupakana tope. Hekima ya mwanamume kamili ni kujua yapi ya faraghani yanayostahili kubanwa.

Tendo la ndoa

Tendo la ndoa lina siri zake ambazo kamwe hazitoki nje ya kuta za nyumba.

Kufichua siri za mwenzio kunaweza kuathiri kabisa uhusiano na kusambaratisha ndoa. Akijua mkeo kwamba yeye ndiye mhusika katika hadithi na ngano za vijiweni, hutamwona wala kumwonja tena.

Usishangazwe akikuacha angalau uwe wa kuliwazwa nao kina yakhe mashabiki wa vijiweni! Na ukija kumla kwa bahati mbaya, utakula shubiri! Hilo nakuhakikishia kwa macho makavu. Kumdunisha mwenzio ni sawia na mume kujivua hadharani!

Najua tabia za uchokozi na uchochezi hasa miongoni mwa baadhi ya wanawake vichwa pumba. Lakini sina shaka uwezo wa stahamala alio nao mwanamume kamili. Anaweza kuhimili matusi, kero na dhihaka za baadhi ya wanawake wenye ndimi za nyoka.

Tahadharini nyie wenye midomo isiyojua kutulia!

Masuala ya huba, kasoro au kupungukiwa maumbile ni siri za moyoni.

Vita, vituko na visa vya chumbani sizo taarifa za habari kuwatangazia kina yakhe na wehu vijiweni.

Migogoro ya nyumbani au tofauti zinazoibuka baina ya wapendanao ni siri zisizopaswa kujadiliwa hadharani.

Jamani sitisheni uchochezi na uchongeaji wa fitina!

Kumsema mwenzio sio hekima bali ulimbukeni. Kimya ni ngao ya mwanamume kamili! Katu mke hawezi kuwa mada vijiweni!

[email protected]