Makala

MWANAMUME KAMILI: Mdharau mwiba, mguu huota tende, corona haitaki mzaha

March 28th, 2020 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

MDHARAU mwiba mguu huota tende.

Hili janga la virusi vya corona si mchezo. Waja zaidi ya kumi elfu wamekwisha agana na ardhi. Tujifunze nini akina sisi tuliosalia? Mbona tunafanyia mzaha hali ya hatari kama hii? Iweje hatusikii wala kusikiliza maagizo ya watalamu? Kuna nini hasa katika vichwa vyetu?

Tunahitaji hamasa na mshawasha wa ushujaa kukabiliana vilivyo na janga hili. Kama jamii, hatuna budi kusoma mengi, tena kwa dharura kufuatia pigo lililofika taifa la Italia. Hebu tuchanganue hali ilivyokuwa nchini Italia wiki chache zilizopita.

Italia ni taifa huru na wananchi wanaishi katika jamii huru huria! Kama ada ya jamii huru, wanakula na kutangamana pamoja. Wanafaana bila mipaka. Wanahudhuria mikutano ya kijamii kama kwamba ni sheria. Wanakongamana maabadani na kwenye mabaa vilevile.

Pamoja na maisha huru huria, ni jamii inayoelekezwa kwa mantiki ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa. Wananchi wanafuata mno maoni na hisia za wanasiasa. Tatizo ni kwamba wanasiasa hawa ni watu “wanaojiamini” ama tuseme “wajuvi wa kila jambo.”

Picha hiyo ya Italia inawiana mno na hali ilivyo hapa nchini Kenya.

Visa vya kwanza vilivyopenya vijijini Italia, hasa maeneo ya Kaskazini, mapuuza waliibuka na kejeli na mizaha kadha wa kadha mitandaoni. Walikejeli virusi vya corona wakivimithilisha na “homa ya mapenzi.” Hawakuona haja kubabaikia “upepo uliopita bila hata kuwapepesa!” Lau wangalijua athari iliyowakabili wasingalifanyia mzaha janga hili!

Isitoshe, watu waliona heri kwenda mikahawani kula na kunywa kama kwamba hapakuwa na hatari yoyote.

Kama ilivyo ada ya wananchi wazembe, walipuuza maagizo ya serikali na kufanyia mizaha mapendekezo, tahadhari na njia za kinga. Walikataa kunawa mikono kwa kuwa “hapakuwa na chakula murua cha Italia!” Waliamua heri kwenda kula “Pizza ya Italia” na kunywa “Cappuccino!”

Wanaume waliona heri kwenda katika baa kunywa na kuvuta “kiko za umma. Waliona heri uhuru wao kutembelea maeneo ya umma kuliko kubanana katika “vikwazo vya serikali.”

Hali ilivyokuwa Italia inamithilika na hali ya sasa hapa kwetu. Tumeambiwa mengi ya kufanya ila hatutaki katu kutii. Tumehimizwa kutojumuika mikahawani, kwenye maeneo ya burudani lakini wapi! Wanawake kwa wanaume wangali kwenye baa na madanguroni wakila vyao kwa raha yao.

Kila uchao maambukizi yanazidi ongezeka na watu hawajaacha chezea shilingi shimoni. Wanywaji wanazidi kunywa huku wakichekacheka na kutematema ya walevi. Wanaopiga chafya wanazidi fanya hivyo vinywa wazi kama mamba walioshiba minofu!

Tumeanza ingiza cheche za siasa katika janga corona. Kuna wale wanaoona mikakati ya serikali kama “njama ya kisiasa tu!” Wengine wanapuuza kwa kuwa “hawajaambiwa na kigogo wa kwao!” Badala ya umoja wa nchi dhidi ya janga hili, tunazidi kuona nyufa na pingamizi kutoka maeneo fulani. Hizi na nyinginezo ndizo changamoto si haba zinazoathiri mikakati ya serikali kudhibiti na kuzuia maambukizi zaidi.

Tumeonywa waziwazi, tumetahadharishwa, tumeelimishwa jinsi ya kujikinga ila tumekataa katakata kuwa waja wenye akili timamu. Kweli, tumekataa. Badala ya kunawa mikono jinsi tulivyoagizwa na vyombo vya dola, tunachekacheka na maji, tunachekeshana kwenye mitandao ya kijamii kama kwamba tumeona amana ya bure!

Haidhuru siku za siku zinajongea! Tutakuja jua nani bingwa kati ya virusi vya corona na mapuuza wanaume kwa wanawake wa leo. Hatuna budi kujifunza somo kutoka utepetevu wa jamii nchini Italia. Mdharau mwiba mguu huota tende.

 

[email protected]