MWANAMUME KAMILI: Mume kamili hawezi kumtoa uhai mkewe

MWANAMUME KAMILI: Mume kamili hawezi kumtoa uhai mkewe

Na DKT CHARLES OBENE

MWANAMUME kamili hawezi kumtoa mwenza uhai kama njia ya kudhihiri ndiye mume.

Badala yake husimama wima kama mkoko akatetea maisha yaliyo hatarini. Hizo ndizo tajriba za mwanamume. Nyie mnaohatarisha maisha ya wenzenu pamoja na gumegume mnaotania wafu ni wanaume sampuli gani?

Hebu tafakari uchungu unaomfika mzazi aliyempoteza bintiye kufuatia uhuni wa wanaume wa leo. Wangapi kati yetu wenye meno ya kucheka tunaweza himili kifo cha binti, mwana uliyemkopoa? Ndio maana sitaacha kuwahimiza kutumia vichwa zaidi ya ndimi zenu. Ndevu sio ishara za mwanamume. Hata mbuzi anazo.

Kila mara panapotokea mkasa na mauti hasa mja kumtoa mwenza uhai, hapakosi mjadala tata. Wapo wanaolaani vikali mauaji na kutaka mkono mrefu wa sheria kuwafikia, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali wahusika. Bila shaka jamii ya wangwana wanaegemea upande huu wa kutekelezwa wajibu wa kisheria. Usije dhani kila mja amesheheni ungwana.

Wapo vilevile wasiojali mno maisha na uhali uliokatizwa ghafla. Upande huu wa mjadala hupenda mno kucheua mambo, kugawa majozi ya lawama, kila mtu ya mzigo wake. Wenyewe wanasema kwamba hakuna mauti yasiyo na chanzo. Sijui kauli yako gani lakini nitakupa maoni yangu bila kuweweseka kope na nyusi.

Binadamu aliyeumbwa akazaliwa kama mimi na wewe ana mamlaka gani kumtoa mwenzake roho? Kama ni chakula chako kimeliwa bila kulipiwa, wangapi wamekula wakakwenda njia zao bila kulipa? Wangapi umewaita wakala shibe yao, jasho kuwatoka, wakakwenda wameshiba mfano wa kumbikumbi? Cha mtu kuliwa ni hali ya kawaida katika dunia hii ya waja kufaana. Ama sivyo? Nionyesheni mtu mmoja katika dunia hii nzima ambaye hajala cha mtu bila kukilipia. Iweje basi kikawa sababu ya mauaji?

Ama ni vita na visanga vya madeni? Kama ni mdaiwa hilo silo sababu. Deni ni nini katika maisha ya mja? Wanadamu ndio wanadaiwa. Tangu lini umemwona mbuzi kahimizwa kulipa deni? Hata akatapo kamba akaingia shambani na kuharibu mali ya mtu, gharama kwa mwenye mbuzi. Hivyo ni kusema kwamba sio tukizi mtu kudaiwa. Nani hana deni? Nani hajawahi kukopa? Mataifa ya ughaibuni yenye rasilimali yanadaiwa sembuse binadamu wanaotapatapa na kubahatisha maisha mfano wa kombamwiko?

Hebu tuyaweke wazi matatizo ya wahuni kuwatokomeza wenzao na kusingizia vijimambo vya kitoto. Mja mwenye kumfuma mwenzake mshale, mwenye kumdunga kisu, ama mwenye kumkata mja shingo alidhamiria kufanya hivyo. Hakuna na wala haitakuwepo sababu nyingine. Maana asingalidhamiria mauaji angaliondoka mbio kama mwoga. Uoga umemwua nani?

Sasa turejelee ule mjadala wa mikekani na vijiweni. Mwanadamu mwenye pumzi hana mamlaka kumtoa mwenza uhai. Kwanza, kabisa tuonyesheni mmoja uliyemfinyanga ukamtia pumzi akawa mtu! Hapo ndipo tutafahamu ukweli kwamba hata wewe mwuaji una uwezo wa kujenga na kubomoa kwa mapenzi yako. Ndio maana nawaunga mkono wangwana wenye kutaka sheria kali dhidi ya wahuni wanaoangamiza wenzao bure.

Nimewahi kusema na nitarejea mkarara ule ule. Mla vitumbua hana budi kudondoa mchele na kusaza chua. Kama hunielewi subiri! Nakuhimiza kutulia taratibu jinsi ulivyosubiri kizindani. Wangwana hawana mapapo. Njia zetu za kobe. Mbinu zetu kama chui kusubiri hadi swara afike puani. Haraka za nini? Uzito wa mwanamume kamili upo akilini wala sio kiunoni.

obene.amuku@gmail.com

 

You can share this post!

FATAKI: Uwongo wa waume ni mwingi; ni jukumu lako kuujua na...

SHAIRI: Kaozwa mapema bila ujuzi