Makala

MWANAMUME KAMILI: Mwanadada usiye na dili naye, afanya nini kwako?

March 7th, 2020 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

SIMBA, kama mwanamume kamili, haondoki nyikani!

Nyie mnaokwepa baada ya nakshi za mahaba ni wale wale tu tuliokwisha kuwazoea.

Nyie wanaume wa leo mwatuvunjia heshima. Mwatudunisha mno kwa zenu raha za kuhubiana na mwishowe kuwakwepa wenzenu kama wenye maradhi.

Acheni niyatoe moyoni angalau msitishe hizi tabia za kuwapachika mimba wanawake ambao hawana haja kulea wala uwezo wa kuwatunza watoto.

Msanii fulani wa muziki wa “Bongo” yuko tena jukwaani! Akina sisi wenye kusema sana ndio kwanza tunaamkia ile habari kwamba “Simba” ameondoka tena! Kweli, “Simba” ameondoka kama ilivyo kawaida yake. Amezoea kutia guu, kuotesha mbegu na kuwaachia mwanamtu ada za malezi tu.

Atatulia lini Simba? Atakomaa lini huyu “Simba” akawa mtu wa kwake? Tabia zake “Simba” zinalandana na tabia za baadhi ya wanaume wa leo. Wametia fora mno kulimbikiza himaya ya vimwana hata mke halali asijulikane nani! Isitoshe, wote wana watoto wanaotaabika kula na kuvaa japo baba zao wako hai! Tunaelekea wapi sisi wenye tamaa kuzaa na kuzalisha kimzahamzaha?

Msinione sura mbovu mkadhani hakunipa Rabana. Wala msidhani raha yangu kununa na kukereka kama sokwe mwingi wa nyege. Nahuzunika mno kuwaona watoto wa watu wakiambulia patupu baada ya kuekeza maisha na nafsi zao katika mahaba!

Mwanamke kushika mimba asiyopangia wala kuhitaji inazidisha hatari ya uavyaji.

Wataavya, mpende msipende! Mimba hizi za kiholela zinachangia pakubwa kuwepo watoto mitaani wanaoishi na kula mapipani. Sio kosa lao kuzaliwa. Ni kosa la mume na mke ambao hawakuchukua tahadhari.

Binadamu wa leo si watu. Wanajua lakini hawataki kujua!

Ni kosa kwa mwanamume kutanguliza tamaa ya kimwili na kushindwa kutumia akili. Ni kosa la mwanamume ambaye kwa kupenda raha ya kufunga magoli hushindwa au hukataa kuchukua tahadhari kuzuia karaha ya matokeo mbaya ya mechi haramu.

Wengi wa wanaume wa leo ni sampuli hii. Wanakula raha na kila jana jike lakini hawataki kamwe kulea watoto ambao ni mazao ya ulimbukeni wao.

Ndio sababu ya kesi mahakamani zisizokwisha. Kukidhia mahitaji ya watoto nje ya ndoa imekuwa kama biashara; kila mmoja akitafuta mnofu mzito sisemi gala la kuchumia. Ole nyinyi wenye kula uroda na kukwepa alfajiri!

Sitazungumzia sana uzembe na ujuha wa baadhi ya kina dada kujipendekeza na kujidekeza kwa wanaume wakijua wazi hatari ya ngono za kiholela! Naambiwa eti ni udhaifu wa kike kushindwa kukataa vya bwerere vikiwemo mimba na magonjwa ya zinaa.

Shauri ni lao! Paka kubeba nundu la ngo’mbe ni ridhaa yake.

Mtu hujikwaa mara moja! Mbona msijue mbinu wanazotumia wenzenu kuwanasa? Mwanamke usiyemhitaji maishani wafanya nini naye chumbani kwako? Nionyesheni mume aliyekufa kwa kupeza huba?

 

[email protected]