Makala

MWANAMUME KAMILI: Tabia njema kwa mwanamume ni kama taa inayotoa mwanga

August 17th, 2019 3 min read

Na DKT CHARLES OBENE

JAMANI nyoka alipewa ulimi tena mrefu kuliko wa mwanadamu.

Sijamsikia nyoka aliyetamba mitaani kutangaza siri za watu.

Wala sijamwona ng’ombe kijiweni akijadili mambo ya nyumba za watu. Hizi tabia za wanaume wa leo zimekuwa kero!

Kila mwenye ulimi ana uhuru kusema na kusemasema anavyotaka. Mtu hakatazwi kutumia vifaa alivyopewa bure.

Lakini tukumbuke kwamba mwanadamu tofauti mno na hayawani. Moja kati ya tofauti hizo ni uwezo wa mja kutambua wapi kuzungumzia wapi kutulia kimya na kusikiliza hekima ya wangwana.

Kunyamaza ni hekima vilevile.

Mwanamume kamili anajua wapi kunyamazia, wapi kuzungumzia. Lakini hawa kasuku wa leo walitoka wapi?

Isitoshe, uwezo wa kudhibiti ulimi hutofautisha mno waja waliokomaa na wale barobaro wanaotaka kutambuliwa mitaani kwa ndimi zinazokiriza kama simu za mkononi.

Ishara za kukomaa mwanamume hudhihiri katika unyamavu wake. Ndio maana nawahimiza wanaume kujifunza hekima na heshima ya kudhibiti ulimi hasa katika makao ya watu wazima.

Tajriba ya mwanamume kamili ni kudumisha mshikamano mijini na vijijini huku kila mmoja akijitahidi kujiepusha na hawaa za nafsi. Kinyume na matarajio ya wangwana; tunaishi miongoni mwa wanadamu wanaopapurana na kulumbana kila uchao kama fisi wanaong’ang’ania mzoga!

Kisa na maana? Mwanamume wa leo mwingi wa ulumbi na ukasuku usiokuza amani nyumbani wala kazini. Hawajui kufunga kinywa na ya mtu kumwachia mtu kujibebea kifuani. Kazi yao kufukua makovu ya watu mfano wa nguruwe atafutaye vimelea topeni. Hizi tabia sio za kiume.

Tatizo ni kwamba udokozi wa mume humwacha mchache wa hekima na ustaraabu. Hizi ndizo kito zinazotofautisha kina yakhe na wanaume wangwana. Isitoshe, ndugu zetu hawana muda kufikiria mambo yao ama kutathmini mipango yao binafsi. Muda wataupata wapi ikiwa kazi yao usabasi na udokozi vijiweni. Si nadra kumpata mwanamume aliyetua miaka hamsini ila hana hanani. Hana jiko hana meko. Hawa wanaume wa kutafuna meno wanaweza kukutia wazimu kabla ya msimu wa kichaa. Tahadharini nyie mnaopenda kupendwa! Mwanamume kamili ni sawa na kilindi cha mto.

Tatizo kubwa linalosibu maisha ya wanadamu wa leo ni uhasama na uadui unaotokana na vinywa vya wanaume visivyodhibitika. Ndio wao hao wanaokimbilia mitandaoni kuchapisha makala na taarifa za maisha ya watu. Mbona muda kupoteza kuchapisha maisha ya wengine ilhali yako huna haja kuipa sura ya maisha mema? Hivi tulivyodhikika maishani, mke yupi mwenye moyo wa jiwe asiyetaka mwanamume mwingi wa ucheshi, umbuji, unyofu, na ucha Mungu? Lakini tuwapate wapi wangwana hao wakati kila mmoja anajitahidi kumpiku kasuku?

Upenyenye na upeketevu wa wanaume wa leo umekuwa ufa unaosambaratisha misingi thabiti ya uchumba na uchu wa mahaba katika nyumba zetu. Na sio ukasuku wa wanaume tu unaochusha maisha ya vichuna wa leo. Wako gumegume wanaopeleka matatizo ya nyumbani au chumbani na kuyaweka mikekani, kujadiliwa na kutafunwa katika mahakama ya malofa wasiojua kitu ila kumwiga mbuzi kuchana majani ya miraa.

Wako vilevile wanaume wanaopenda sana kuanika matatizo yao kwenye mitandao ya kijamii angalau kutafuta huruma na ushauri kutoka wajuvi wa mambo mitandaoni.

Chumba kina heshima zake. Wapendanao na wanandoa wanaweza kupigana kumbo chumbani lakini wakajitokeza na miale ya tabasamu na uchesi usiomithilika.

Kwa hekima hiyo, inakuwa vigumu mahasidi kupenyeza pua zao kwenye siri za familia. Hebu wajibikeni nyie mnaoshinda mitandaoni kuchapisha makala na taarifa ya maisha binafsi. Hatuna haja kujua shida zenu.

Zetu dhiki zinatosha, tena mzigo zaidi! Kila pweza na mchuzi wake!

Tabia njema kwa mwanamume ni kama taa inayomwaya mwanga. Mwanamume kamili sharti kudhihiri wema uliokita moyoni mwake. Hakuna wema katika udokozi na usabasi mitandaoni. Isitoshe, mwanamume anahitajika kushawishi watu kuiga maadili yake. Tutaiga nini kwa watu wasiojua hekima ya mwanamume kunyamaza na kupima mambo ya kunena katika hadhira? Usharifu ndio uume hasa!

Hebu niwajuze nyie walumbaji. Visa vidogovidogo vya kutuliziwa pajani havina haja kumwagwa kwenye kuku wengi vijiweni, mitaani na mitandaoni. Mwanamume kamili mwingi wa utundu. Anapendeza mno kwa weledi wake kuzichezesha shanga na tunda kiunoni mwa mpenzi, au mkewe! Kusemasema tumwachie kasuku.

Sisi ni waja wenye hekima na akili razini. Isitoshe, dunia yenyewe moto wa kuotea mbali, mbona basi kutiliana chumvi kwenye madonda-ndugu?

 

[email protected]