Makala

MWANAMUME KAMILI: Tusijitie hamnazo suala la uzazi

July 4th, 2020 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

DUNIA haina shukrani! Ole nyinyi mnaojituma kufa kupona wenzenu kuwapa nafsi na moyo vilevile! Sikateni tamaa wala kushika tama na kusononeka kwa tabia za wafidhuli wanaume wa leo.

Kutojua jambo sio ujinga; ujinga ni kukataa katakata kujifunza! Hivyo ndivyo walivyosema wazee wa jadi weledi wa mambo.

Kuna baadhi ya wanaume wenye akili za nanga hata kujifunza ni kazi.

Uzito huu wa akili unatokana na tabia za wanaume wa leo kutopenda kujuzwa ya hekima. Wanajifanya kujua kila kitu. Hawaambiliki hawasemezeki!

Kuna mengi ambayo wanaume wa leo wameyafumbia macho na kujifanya hawajui! Kweli sijaelewa jinsi mwanamume anavyoweza kupachika mimba na mwishowe kukataa kuwajibikia malezi ya mwanawe akitilia shaka asili na fasili ya mtoto yule.

Vipi mtu kutilia shaka uzao wa mtoto katika dunia hii ya teknohama? Hivyo ndivyo alivyofanya dume moja kwa takriban miaka ishirini hadi alipohusika katika ajali barabarani na kuachwa mahututi!

Wanaojua ukweli waliniarifu kwamba miaka ya nyuma, jamaa yule alihusika kimapenzi na binti mmoja ambaye walikosana na kutengana naye punde tu baada ya kidosho kuhimilika. Wajua tena akina sisi tunaopenda kula vya watu tukipita. Yaani akina sisi tunaopenda kupitiapitia tu. Huwa hatuna haja kabisa kujua kulizuka nini kisogoni. Sijui tabia hizi tutazizika lini? Tuzame wapi akina sisi wenye haya usoni?

Licha ya kwamba alikuwa mwanamume msomi, alikataa katakata wazo kwamba ile mimba ilikuwa yake. Mwisho wa siku alikana mwana na kizinda. Kwa miaka zaidi ya ishirini, mtoto alijaribu kila njia kujitambulisha kwa babake mzazi lakini dume lile lilimkana.

Ya Rabana ni mengi. Baada ya miaka mingi ya dhiki, baba na bintiye walikutanishwa tena hospitalini katika hali ya kusikitisha. Mzee alikuwa mahututi hana hanani, hatima yake mikononi mwa muuguzi akiwa ndiye yule bintiye aliyemkana miaka ya nyuma. Mengine nawaachia nyie wambea kuyaendeleza mkekani.

Huwa wapi hawa wanaume wanaoibuka na kuwakana watoto wakijua wazi walifanya mambo ya wakubwa? Ama ndio nyie mnaojua kupanda ila kuvuna. Ndio wao hao wanaopanda kitandani na madaftari ama majadala kuyasoma wakati watu wazima wanakuwa shughulini.

Ndio wao hao wanaopokea simu na kujadili biashara kwa lisali moja tena usiku wa manane wakiwa juu ya mnara. Ndio wao hao wanaokesha mitandaoni ya kijamii ilhali wanawajibikia shughuli za watu wazima.

Jamani zindukeni nyie wenye kuwafanyia wenzenu dhihaka kama hizo!

Inachukiza mwisho wa chuki mtu kukufanyia dharau sampuli ile. Mwenzio kajisabilia kwako mwili na nafsi, fikra na akili, pumzi na uhai wala huoni haja kumpa hata tone la heshima?

Madaftari na majalada ya kusomwa usiku wa manane ndio heshima? Ndio heshima anayostahili mke kwa kukuchagua wewe na kukufanya mtu mbele ya watu? Nyie wanaume wa leo mna nini? Afadhali mwenye kukupa talaka kuliko mwanamume apandaye kitandani na rununu na kujadili biashara wakati mkewe anasubiri kupanda wanakopanda waliojazibika kimahaba! Afadhali mtu kusalia peke yake maishani kama mwezi kuliko kudunishwa namna ile.

Nani kawaambia wanawake hawana biashara ama hamu ya kusoma majalada na madaftari kitandani? Hebu kivalie kiatu cha mwenzio kabla kumdunisha namna ile. Tabia hizi hazina nafasi katika meza wa watu wanaothamini wenzao.

Tulivyo wachapa kazi, baadhi yetu tunasingizia shughuli aina ainati kama sababu ya kupitwa na mengi ya chumbani na vilevile nyumbani.

Ukweli ni kwamba baadhi yetu ni wanaume limbukeni tusiopenda kujituma kimaisha na kujua mambo yanayohusu mke. Ndio maana wanaume wa leo hawachelei kukana watoto kama kwamba hawakuhusika walivyohimilika mama yao.

La ajabu ni kwamba hata kuuliza siku za hedhi tunaona kama kazi ya sulubu. Wanaume wa leo kazi yao kukabana koo tu.