Makala

MWANAMUME KAMILI: Ubaguzi wa nini ilhali sote tumezaliwa namna moja?

September 7th, 2019 3 min read

Na DKT CHARLES OBENE

NZIGE wana huruma kuliko wanawadamu wa leo!

Karibu nikujuze kinaya ya wanadamu kula pamoja gizani lakini kubaguana mchana wa jua.

Licha ya dunia kujaa vimwana warembo mfano wa lulu na madume wenye vifua na misuli tingi’nya, hatujaondokewa na ule wasiwasi wa “wanawake kukosa waume na vilevile wanaume kukosa wanawake wema!”

Wengi wanashangaa vipi njaa kushadidia wakati wa mavuno? Vipi ukame kushamiri wakati wa masika? Hili joto la kukosa wachumba linazidi kuteketeza mili ya wengi licha ya msimu wa kipupwe.

Kulikoni nyie mnaotafuta msiwaone wanawake na wanaume katika nyika iliyojaa kila aina ya jaala? Mnatafuta nini hasa kando na watu wenye utu? Nielezeni nipate elewa bayana sifa mnazotafuta ambazo mmeshindwa kuzipata katika wangwana waliojaa na kupwa duniani.

Kwanza, tukubaliane kwamba licha ya utandawazi na jitihada zote zinazolenga uhamasishaji umma, bado hatujaondokewa na lile jinamizi la ubaguzi. Tunabaguana hadi kwenye vyumba na vitanda vyetu.

Ubaguzi huu haupo kwenye masuala ya mahaba na ndoa pekee.

Matabaka (wengine wanasema tu tabaka hata kwa wingi) yanazidi ibuka kila uchao.

Si kazini si vyuoni si maabadani si madanguroni si serikalini si mitaani.

Sampuli ya “watu wema” wanaona wenzao “si kitu wala watu” wanaostahili utu na heshima. Hata wanasiasa wamekwisha anza kuchochea hisia kwa kujitambia “ulalahoi” japo wenyewe wanaishi katika mitaa ambayo kumwona nzi ni tukizi. Tangu lini “walalahoi” wakaishi na kutangamana katika mitaa ya Karen, Muthaiga, Kitsuru, Runda, Peponi na mengineyo ya kifahari kama hayo?

Hakuna siri kwamba wanawake kwa wanaume wa leo wanabaguana kwa misingi tofauti. Si kabila, si tabaka, si daraja la elimu, si umaarufu wa jamii, si rangi ya ngozi, si ukwasi wa wazazi ama jamii, si kazi wanazofanya watu.

Kundi moja la kina mama lilikutana hivi maajuzi “kupinga moja kwa moja mwanao kuolewa na jamii ya wavuvi!” Hapo ndipo nilipotambua kwamba nzige wana huruma kuliko binadamu wa leo. Ningependa kuwakumbusha kina mama wale kurudia lile somo la dini angalau kujikumbusha kwamba wafuasi wa kwanza wa Mtume Yesu walifanya kazi ile ile ya uvuvi.

Kinaya ni kwamba wenye navyo wanaona haya kutangamana mchana na kina yakhe walalahoi wanaobahatisha maisha jinsi mende wanavyobahatisha maisha kusubiri posho kwenye mwiko. Lakini subiri ujionee maajabu ya gizani katika mitaa, vijia na vilabu vya mahaba! Ajabu ni kwamba hizi tofauti za tabaka katu si kikwazo gizani. Mara ngapi tumesikia visa vya mwinyi wanaoshukiwa kuatika mbegu katika mashamba ya waajiri bila idhini ya wenye shamba?

Nilikuwa mahakamani wiki jana kusikiliza kesi iliyomkabili bwanyenye mmoja aliyeasi malezi ya mwanawe – mwana wa kuzaliwa na mjakazi! Isitoshe, akina sisi tunaokula na kulala mapipani ni watoto tuliozaliwa katika koka zilizojaa nguvu, mamlaka, madaraka utajiri ila baba zetu wanatuonea haya wasitake hata kutambuliwa nasi. Vipi matajiri hawa kuona fahari kula raha na mama zetu lakini wasione haja kutangamana nasi tunaoitwa mbegu mbovu?

Kama kweli tabaka zipo kutofautisha watu, mbona matajiri wakala raha na kuzaa na masikini? Mbona wasomi waatike mbegu zao katika vijishamba vya akina yakhe wasiojua hata kufungua ukurasa na kitabu cha maisha? Binadamu kwa kujaaliwa mengi na mema wamesahau kwamba mtu hachagui uzao wala ulezi, hachagui ufukara wala ukwasi. Sote tunazaliwa namna na jinsi moja.

Tufanyeje akina sisi ambao urathi wetu ni ufukara miaka nenda miaka rudi? Nani mwenye kutuona na kutufaa kimaisha? Tuolewe na tuoe nani?

Hata tukipenda tunaambiwa waziwazi kwamba hatujatosha kitoweo! Tukipendeza, tunazomewa na kukashifiwa kujipendekeza kusikotufaa!

Wanaobagua wenzao wanasahau kwamba maisha, kama mto hufuata mkondo! Licha ya kuzaliwa maeneo kavu na tambarare, kuna wanawake kwa wanaume waliojizatiti kubadili maisha na sasa ni watu tajika. Isitoshe, wako vilevile watoto wa matajiri wenye bongo zisizoshika kitu! Mbona sasa kubaguana?

Umoja, chudi, bidii na mapenzi ya dhati ndizo njia za pekee zitakozowapa wanadamu mwanga wa kuona wema miongoni mwao. Dunia ya leo inahitaji wanadamu wanaochukuliana mizigo na kufaana kimaisha. Hao ndio watu wanaonipa hamasa na kunishawishi kujibidiisha angalau niondoke miongoni mwa umati uliokubali kufa nyonyo na macho.

Natamatisha kusema kwamba sitaki kuishi na vipofu wa akili, nafsi na ari.

Natamani kuwa mtu mbele ya watu! Ndio maana nahamakika wanadamu wanapobagua wenzao hadharani.

Mwanamume na mwanamke kamili hana haja kuwabagua wenzake kwa misingi ya tabaka, kazi, ukwasi, ama kimo! Kufanya hivyo ni kukosa utu.

 

[email protected]