Makala

MWANAMUME KAMILI: Uongo umeua mapenzi, epuka!

June 27th, 2020 2 min read

Na DKT CHARLES OBENE

KUNA baadhi ya wanaume kwa wanawake wa leo wasiojua adabu wala heshima kwa mwenza.

Yaani unawapa kila kitu! Si nafsi si moyo lakini bado hawaridhiki! Umekwisha kuwapa vyote vya kupewa mtu lakini bado wanataka usuhuba pembeni.

Raha yao kulimbikiza himaya ya marafiki wasiojua mipaka ya mzaha. Jamani mnataka nini duniani nyie wenye tabia hizi duni? Mwanamume kamili sharti kujua mwisho wa mzaha.

Mara kwa mara ninaona tabia za wanaume kuficha simu zao usiku ama wengine wanazima kabisa! Wengine nao wanaona heri simu kulazwa kifudifudi, uso na mwanga wake usionekane!

Sijui na sitaki kujua sababu ya tabia hizi za baadhi ya wanaume wa leo. Nijuavyo ni kwamba siku za mwizi ni arobaine.

Hakuna mke akijua thamani yake vyema atavumilia usumbufu wa nje mara kwa mara.

Usiku wa manane simu kukiriza ni ishara ya nyumba isiyokwisha dhiki. Ni ishara ya mchezo wa paka na panya tu. Nyumba na chumba haishi adabu na heshima. Sharti mume na mke kukomaa na kujua ukweli huu.

Wekeni mipaka ya mzaha nyie mnaotaka usuhuba na dunia nzima!

Mtu kukupa moyo na nafsi yake nawe usione heri kumpa japo heshima? Kwa uchimvi huu mtasalia na hadithi za paukwa pakawa miaka na mikaka!

Nani mwenye kulaumiwa kwa kosa la uongo kushamiri katika uhusiano au hata nyumbani baina ya mke na mume?

Nazo ndimi zenu zinanena nini kuhusu uhalisi wa mambo ambayo si dhahiri kwa jicho la pembeni?

Hekima ya uwazi ina msingi kwamba wanadamu wanastahili kuyaweka wazi ya wazi hata kama yanaweza kumtoa mtu roho. Hii ni kwa sababu wanyonge huanza safari kwa subira na uvumilivu.

Ndani mwa subira na uvumilivu wao ndimo mnaoishi kani na nishati zinazokuza imani. Nao mche wa uwazi ndio mti wenye shina uitwao imani.

Hata hivyo, unyonge wa wanaume kwa wanawake wa leo unamithilishwa na ule uwezo wa mkia wa mbuzi kuzificha siri za mbuzi.

Kujizatiti kumfundisha mwanadamu umuhimu wa uwazi maishani ni kazi – tena kazi ngumu kama kumwelewesha chizi. Nao machizi ndio kwanza wamezuka kutoka majaa walimojaa tayari kutwaa yadhifa za uongozi nyumbani na chumbani.

Heri wazee wa kale. Angalau walijua wapi kufunguka kinywa na wapi kukifyata! Walipendeza kwa jinsi walivyouweka ukweli bayana ili kila mja atwae mzigo wake. Kwao, neno lilikuwa sawa na deni kubwa lililoweza kuzoa fedheha kuliko deni la fedha. Ndio maana wazee wa kale walidhihiri ungwana. Kwa ungwana wao, walipendwa sana tena waliwajibikiwa mno na wanawake wa kale.

Tatizo langu ni hizi tabia hadaa za wanaume kwa wanawake wa leo. Kutongozana kazi nzuri lakini tuifanye kwa msingi wa ukweli, uwazi na heshima. Jamani wanaume tuache kujidunisha kulimbikiza himaya ya wakeketeji pembeni na kuwaachia uhuru kuwapigia simu usiku wa manane!

Binafsi siwezi kumridhia mtu; awe mke ama mume kunidunisha ningali mtu wa pumzi.

Uwazi ni sifa ya mwanamume kamili. Jamani wanaume wa leo mnachosha wake na wakeketaji wenu! Hizi tabia zenu kujificha kivulini ndizo zinawaelekeza katika usuhuba na pwaguzi wezi na mali na miili.

Isitoshe, mwanamume akipenda kitu – ama – kitu kikimpendeza, haoni aibu kujizoazoa juu kwa juu na kudhihiri alivyofurahishwa nacho. Ukipendwa pendeka! Nayo macho ya pembeni yazibe usione wala kusikia ya pembeni.

Kuna nini pembeni ambacho mtu hana kwake nyumbani?

Adhabu ya mume wa karne hii ni kumchumbia mke mmoja! Kitanda kimoja na bega moja! Asione hata shanga ila za mmoja ambaye amekwisha kumpa heshima na kumfanya mtu mbele ya watu.