Habari Mseto

Mwanamume kulipa faini ya Sh100,000 kwa kuiba mananasi Delmonte

February 27th, 2024 1 min read

KENYA NEWS AGENCY NA ALEX NJERU

MWANAMUME ameagizwa kulipa faini ya Sh100,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kuiba mananasi 42 katika shamba la Delmote mnamo Februari 23.

Alex Ndung’u alifika mbele ya Mahakana ya Kenol na kukiri kuiba mananasi hayo ya Sh4, 200.

Hakimu Mkazi, Jackinda Rennah, alielezwa na upande wa mashtaka, kuwa si mara ya kwanza kwa mshtakiwa kushiriki uhalifu.

“Mwaka 2022 katika Mahakama ya Kandara na Kenol mwaka 2023, mshtakiwa alihukumiwa kwa makosa sawia na hili,” akasema kiongozi wa mashtaka.

Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kathwana, Kaunti ya Tharaka Nithi walikesha nje usiku kucha, baada ya upepo mkali ulioandamana na mvua kuharibu paa za nyumba zao.

Tukio hilo lililotokea Jumatatu, saa nne usiku, liliharibu majengo ya kituo cha mafuta, Kanisa Katoliki, mkahawa na baadhi ya maeneo ya soko la Manispaa ya Kathwana.

Padri wa Parokia ya Kathwana, Bw Gerald Mugendi alisema upepo huo uliharibu choo, jikoni na jengo jipya la kanisa hilo.

“Tunakadiria hasara kubwa. Tunaomba serikali ya kaunti na kuu kutusaidia kutokana na janga hili,” alisema Bw Mugendi.

Hata hivyo, hakuna majeraha yaliyoripotiwa kutokana na janga hilo.