Mwanamume kulipwa Sh700,000 kwa kulea mtoto ambaye aligundua baadaye si wake

Mwanamume kulipwa Sh700,000 kwa kulea mtoto ambaye aligundua baadaye si wake

Na PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA Kuu mjini Mombasa imeagiza mwanamume alipwe Sh700,000 kwa kumlea mtoto ambaye aligundua baadaye kuwa si wake.

Iliamuliwa pesa hizo ambazo ni fidia kwa mateso ya kiakili na gharama ya malezi zitalipwa na baba halisi wa mtoto huyo wa kike.

Katika uamuzi ambao ni wa kipekee, mahakama hiyo iliamuru mwanamume huyo aliyetambukiwa kama Bw SVK, alipwe Sh400,000 kama fidia kwa msongo wa mawazo na vilevile kufedheheshwa katika jamii.

Sh300,000 ni alizotumia kugharimia mama mtoto wakati akiwa mjamzito na kwa gharama ya mke wake kujifungua hospitalini.

Jaji Eric Ogola alimtaja Bw SVK kama mtu muungwana ambaye alimpeleka mke wake, ambaye sasa wameachana, hospitalini kujifungua na kulipa gharama lakini mwanamke huyo aliamua kwenda kwao ambapo alimwambia Bw SKV habari za kuvunja moyo kuwa hakuwa baba ya mtoto huyo.

“Kwa shida hizo zake zote, Bw SVK anastahili kufidiwa kwa gharama aliyoipata kwa kumuangalia mama na mwanawe,” alisema Jaji Ogola.

Baraka ya mtoto

Bw SVK katika stakabadhi zake za kesi alisema kuwa, alikuwa mume wa Bi RNL na walikuwa wakiishi pamoja kama mume na mke na katika uhusiano wao, wakabarikiwa na mtoto wa kike aliyezaliwa Oktoba 2015.

Aliiambia mahakama kwamba alilipa gharama zote za mke wake kujifungua hospitalini na kununua nguo na vitu vyote vilivyohitajika kwa ajili ya mtoto aliyezaliwa.

Alisema alijivunia kumpata mtoto huyo hadi akaamua kumuita jina la mama yake.

Hata hivyo, RNL alimpigia simu mnamo Septemba 2016 akiwa kwa wazazi wake na kumwambia kuwa hakuwa baba wa mtoto huyo.

Kwa kutoamini, aliamua uchunguzi wa kisayansi wa DNA ufanywe kwa mtoto huyo, jambo ambalo Bi RNL alikubali.

Uchunguzi wa DNA ulifanywa Afrika Kusini, ikabainika kuwa hakuwa baba wa mtoto huyo.

Katika upande wake, baba halisi wa mtoto, aliyetambulishwa kama NTA, ambaye sasa wameoana na mwanamke husika, alisema mnamo 2015 alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bi RNL lakini ulikatika baada ya mwanamke huyo kuolewa na SVK na wakabarikiwa na mtoto.

Alisema aliwasilisha kesi mahakamani ili haki zake kama baba mtoto kuthibitishwa na kutaka jina la kati la mtoto huyo kubadilishwa.

Mahakama iliamuru msajili wa maelezo kuhusu vifo na kuzaliwa mjini Mombasa arekebishe cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo katika sehemu ya baba.

You can share this post!

Uhuru awafinya mawakili

Makanisa Kiambu yajiandaa vilivyo kuwapokea waumini

adminleo