Kimataifa

Mwanamume kuozea jela miaka 5,000 kwa mauaji ya halaiki

November 22nd, 2018 1 min read

MASHIRIKA naa PETER MBURU

MAHAKAMA moja ya taifa la Guatamela, Amerika ya Kati imemhukumu mwanaume aliyekuwa mwanajeshi miaka ya zamani kifungo cha miaka 5, 160 gerezani baada ya kumpata na hatia ya mauaji ya halaiki, wakati wa vita vilivyokumba taifa hilo miaka ya themanini.

Mahakama hiyo mnamo Jumatano ilimtupa jela Santos Lopez kwa miaka 30 kwa kila kati ya mauaji ya watu 171 yaliyotendeka, kwa jumla ikiwa miaka 5, 130.

Mwanaume huyo aidha alifungwa miaka mingine 30 katika kesi aliyohusishwa na mauaji ya mtoto.

Lopez alikuwa kati ya wanajeshi waliotumwa kuzuia ghasia waliopewa mafunzo na Marekani katika kikundi kilichoitwa Kaibil na alikamatiwa US na kurejeshwa katika taifa hilo mnamo 2016.

Uchunguzi ulibaini kuwa Lopez alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa kupiga doria ambao walitekeleza mauaji hayo mnamo Desemba 1982 katika eno la Dos Erres, katika mpaka wa Mexico.

Wanajeshi hao walikuwa wakijaribu kutwaa bunduki 20 ambazo zilikuwa zimeibiwa na wanamgambo wakati walipovamiwa na 19 kati yao wakauawa.

Baadhi ya wanajeshi wengine wa kikosi hicho wamehukumiwa mbeleni na wote walifungwa zaidi ya miaka 6,000 gerezani.

Wengine bado wanadaiwa kuwa wako US hadi sasa.

Mauaji hayo yalitendeka wakati wa utawala wa Efrain Rios Montt, ambaye pia alishtakiwa kwa makossa ya mauaji ya halaiki, kabla ya kufariki mnamo Aprili mwaka huu.

Montt alidaiwa kuamrisha watu 1, 771 kutoka jamii ya Ixil-Maya wauawe wakati alipoongoza taifa hilo kati ya 1982 na 1983, mauaji ya watu wengi zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya miaka 36 ambayo vita vilipiganwa nchi hiyo.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, takriban watu 200,000 waliaga dunia ama waliuawa wakati wa vita Guatamela, ambavyo viliisha mnamo 1996.