Habari Mseto

Mwanamume ndani kwa kukatakata mtoto wa kambo kichwa

June 19th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Polisi eneo la Timboroa wanamzuilia mwanamume mmoja baada ya kumkatakata mwanawe wa kambo kwa panga kichwani, kisha kumfungia chumbani aipate matibabu.

Mshukiwa, Bw Kuria Kimungu anadaiwa kumkatakata mvulana huyo wa miaka kumi mara kadhaa kichwani na kumjeruhi vibaya mnamo Juni 6.

Kulingana na majirani, mshukiwa baada ya kutenda uovu huo alimfungia mtoto huyo wa darasa la tatu chumbani katika boma lao, kijiji cha Shauri, ili isifahamike.

Hata hivyo, walimu walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiumia baada ya kwenda shuleni siku ya Jumatano, ndipo akapelekwa kupokea matibabu kwenye kituo cha afya kilichoko eneo hilo.

Mwanamume huyo alikamatwa baadaye na kufungiwa seli katika kituo cha polisi cha Timboroa.

“Mamake mtoto huyo alitoroka baadaye na anatafutwa na polisi kwani hakuripoti kisa hicho cha mwanaye kudhulumiwa,” akasema Bw Stephen Chege, jirani.

Sasa, mtoto huyo pamoja na ndugu zake wawili wamebaki bila mlezi.

Kisa hiki kilitokea wiki mbili baada ya mwanamume mwingine katika kijiji hicho kumtia bintiye wa miaka 15 mimba, kisha kutoroka kukwepa mkono wa sharia.

Baba huyo anasemekana kuwa na hulka ya kufanya tendo la ndoa na mwanawe wa darasa la nane hadi siku ya 40 ambapo alimpachika mimba, ndipo ikajulikana.

Mtoto huyo sasa hajakuwa akihudhuria masomo, japo anatarajia kufanya mtihani wa kitaifa wa KCPE mwishoni mwa mwaka huu.

Chifu wa eneo hilo Bw Jacob Njehia amewaonya wazazi wanaotelekeza majukumu ya ulezi na wale wanaowadhulumu wanao kuwa serikali haitachelea kuwaadhibu kisheria.