Habari Mseto

Mwanangu alifumaniwa akifanya ngono na shangaziye, mwanamke aambia korti

February 7th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MVULANA mwenye umri wa miaka 26 aliyenusurika shambulizi la polisi katika bustani ya Citi Park mwaka uliopita ameelezea jinsi shangaziye alivyopigwa risasi na kuuawa papo hapo.

Na mama yake Benard Chege Gathima , alimweleza Jaji Stellah Mutuku kuwa, anasononeka sana kwa vile mwanawe alifumaniwa akifanya ngono na shangaziye katika bustani ya Citi Park, Nairobi.

“Mimi ninasononeka sana kwa vile niliambiwa mtoto wangu alikutwa akifanya mapenzi na mke wa mjomba wake. Walikutwa wakiwa uchi,” Bi Faith Wangui alimweleza Jaji Stellah Mutuku anayesikiza kesi ya mauaji dhidi ya maafisa wawili wa polisi William Kipkorir Chirchir na Godfrey Kipng’etich Kirui .

Maafisa hawa wawili wameshtakiwa kwa kwa kumuua Janet Wangui Waiyaki mnamo Mei 20, 2018.

Akitoa ushahidi, Chege alisema alipigwa risasi na kupata majeraha mabaya.

“Tulikuwa tumejifungia ndani ya gari mimi na Janet katika bustani ya Citi Park baada ya kuwasili kutoka Naivasha. Mimi nilisinzia kwa uchovu naye Janet alikuwa amelala. Nilisikia gari likigongwa gongwa. Nilirudisha gari nyuma na kuchomoka ndipo nikasikia uchungu kiunoni baada ya kumsikia Janet akipiga duru kwa uchungu,” alisimulia Chege.

Jaji Mutuku alifahamishwa gari la Chege liliingia ndani ya mtaro na maafisa wa polisi wakafika mahala pale.

Alieleza wakiwa ndani ya mtaro alimwita Janet aliyekuwa amemlalia kisha akanyamaza.

“Nilifungua mlango nitoroke lakini nilikuwa nimepata majeraha,” alisema Chege.

Aliendelea, “Afisa mmoja alimwinua Janet kisha nikasikia akiuliza huyu kweli yuko nasi (akimaanisha Janet).”

Chege alisema wakati huo alikuwa anavuja damu jingi na alianza kuzirai.

“Afisa mmoja wa polisi aliniuliza nataka kupelekwa hospitali ipi? Aga Khan, Kenyatta ama Avenue?” Chege alikumbuka.

Chege alisema alipelekwa Avenue na kulazwa mle. Habari za kupigwa risasi kwa Janet zilisambaa haraka na marafiki wakamtembelea hospitali.

Alisema Janet alilipuliwa na risasi. Akihojiwa na wakili Ham Langat, Chege alisema haoni ubaya wowote kukesha na shangazi yake.

“Je, huoni makosa ya kufanya tendo la ngono na mke wa mjomba wako, Bw George Gathumbi,” wakili Ham Langat alimwuliza Chege.

“ Sioni ubaya wa kuwa naye. Tulikuwa marafiki,” alijibu.

Ushahidi huo wa Chege ulishangaza kila mmoja mahakamani aliposema “ sioni ubaya wowote wa kukesha nikiwa na mke wa mjambawe.”

Siku hiyo ya Mei 20 2018, Chege alisema polisi waliwavamia katika bustani ya Citi Park na kuwamiminia risasi bila sababu na kupelekea mkewe mjomba wake kuaga.

Chege alisema waliondoka na Janet Mei 19 2018 kuenda Naivasha ambapo walikesha usiku kucha.

“Kabla ya kwenda Naivasha tulishinda katika kilabu kimoja Pangani tukiwa na Janet na rafiki yangu kwa jina Koome,” Chege alifichua mienendo yao.

Mvulana huyo alisema walikuwa wakitafuna miraa na kubugia pombe.

Kesi inaendelea Feburuari 19 , Chege atakapohojiwa zaidi.