Michezo

Mwanariadha Alex Korio apigwa marufuku na IAAF

July 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KITENGO cha Maadili (AIU) cha Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kimempiga mtimkaji Alex Korio Oloitiptip marufuku ya miaka miwili kwa kukiuka kanuni zinazodhibiti matumizi ya pufya.

Korio, 30, alikuwa amepokezwa marufuku ya muda mnamo Mei 2020 baada ya kubainika kwamba alikosa kujitokeza kupimwa mara tatu ili kubaini iwapo aliwahi kutumia dawa haramu za kusisimua misuli.

Ingawa alipewa nafasi ya kujitetea, ushahidi aliowasilisha haukusadikisha wanajopo wa AIU.

“Korio alikosa kufanyiwa vipimo vya afya mara tatu mfululizo chini ya kipindi cha miezi 12. Hilo ni kosa ambalo humpa mwanariadha yeyote marufuku ya moja kwa moja. Isitoshe, alikataa kujibu barua tulizomtumia wala kutoa maelezo yoyote tulipotaka kujua kiini cha kukosa kwake kupimwa,” ikasema sehemu ya taarifa ya AIU.

Adhabu ya Korio ambaye amepania kukata rufaa, inaanza kutekelezwa mnamo Julai 19, 2019 hadi Julai 19, 2021.

Mbali na marufuku, Korio anapokonywa pia alama, mataji na tuzo za medali na fedha alizojinyakulia kwa kuibuka mshindi wa mbio zote alizozishiriki kuanzia Julai 2019.

Mtimkaji huyo wa KDF aliwakilisha Kenya katika mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mwaka jana na akaambulia nafasi ya 11.

Anakuwa Mkenya wa 55 kupigwa marufuku na AIU chini ya kipindi cha miaka mitano.

Anaungana sasa na bingwa wa Olimpiki Jemima Sumgong, bingwa wa Boston na Chicago Marathon Rita Jeptoo, bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop.

Korio anaadhibiwa siku chache baada ya mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Wilson Kipsang, kupigwa marufuku ya miaka minne kwa msururu wa makosa ya kukiuka kanuni zinazodhibiti matumizi ya pufya na kuwasilisha ushahidi wa uongo wakati wa kujitetea.

Mwaka huu pekee, wanariadha watano wa Kenya wakiwemo Kipsang, Alfred Kipketer, James Kibet, Mercy Jerotich na Kenneth Kipkemoi, wamepigwa marufuku kwa makosa ya kutojitokeza kufanyiwa vipimo vya afya.

Waziri wa Michezo, Amina Mohamed amesema Serikali inapangia kupitisha sheria itakayoshuhudia wanamichezo wanaotumia dawa za kusisimua misuli wakiadhibiwa vikali kwa kiwango sawa na wahalifu wengine wanaofungwa jela kwa makosa ya jinai.

Amina amefichua kwamba wizara yake inashirikiana vilivyo na shirika la kukabiliana na matumizi ya pufya nchini (ADAK) kuandaa mswada utakaowasilishwa bungeni kwa mjadala.

“Tunatarajia mswada huo ukamilike katika kipindi cha miezi miwili ijayo. ADAK pia wanatayarisha mapendekezo ambayo tutatekeleza pindi watakapotuwasilishia,” akasema Amina.

Huku visa vya matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha wa Kenya vikiongezeka zaidi chini ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, Amina ameshikilia kwamba wamejitolea kukomesha kabisa uozo huo na kuhakikisha kuwa wanariadha wa Kenya wanatamba katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa bila ushindi wao kutiwa doa.

“Tunalenga sana kuhifadhi hadhi ya taifa letu. Kenya ni ngome ya wanariadha wa haiba kubwa ambao wamekuwa wakitikisa ulimwengu kila mwaka kwa mafanikio yao ya kutamanisha bila kutumia dawa. Hivyo, hatutaki jina la Kenya lipakwe tope zaidi ulimwenguni kwa sababu ya watu wachache wabinafsi wanaopania kutumia njia za mkato kujitafutia ufanisi,” akashikilia Amina.

Kenya iko katika kategoria ya kwanza (A) ya mataifa ambayo wanamichezo wao wanatumia sana dawa haramu ili kujipatia ufanisi kwa njia za mkato. Nigeria, Ethiopia, Bahrain, Morocco, Ukraine na Belarus ni mataifa mengine katika kategoria hiyo.

Kenya imekuwa ikimulikwa sana na shirika la kupambana na pufya duniani (WADA) pamoja na IAAF kutokana na kukithiri kwa visa vya matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha wake tangu 2012. Tangu mwaka huo, zaidi ya watimkaji 40 wamepigwa marufuku. WADA imefichua kuwa wanariadha 138 kutoka Kenya wamewahi kutumia pufya kati ya 2004 na Agosti 2018.